Na Mwantanga Ame,Dodoma
KAMATI za Bunge Maalum la Katiba, zimepinga ukomo wa kushika nafasi za ubunge, kama ilivyopendekezwa katika rasimu ya katiba na kutaka mfumo wa sasa uendelee.
Mwenyekiti wa Kamati namba 2, Shamsi Vuai Nahodha, aliwasilisha maoni ya wengi jana katika sura za tisa na 10, alisema ameamua kufanya mabadiliko ya sura hiyo, kwa kuondoa ukomo wa kutumikia nafasi hiyo kwa vipindi vitatu kama ilivyopendekezwa na rasimu na badala yake liwachwe liendelee kama ilivyo sasa.
Alisema Tanzania inafuata mfumo wa kidemokrasia na haitakuwa busara uhuru huo ukabanwa pale watu wachache watakapoona kwao ni sawa kumuondoa mbunge huyo.
Alisema mabadiliko mengine ambayo kamati hiyo ilipinga ni ushikaji wa nafasi pale Mbunge aliyechaguliwa atakapoondolewa ama kufariki kwa nafasi yake kushikwa na mtu alieshika nafasi ya pili.
Alisema hatua hiyo inaweza kuzua visa vya makusudi, kwa mtu ambaye alishika nafasi ya pili ambaye anaweza kufanya jambo lolote litakalochangia kuondolewa kwa mbunge aliechaguliwa.
Maeneo mengine ambayo aliyataja kufanyiwa marekebisho ni kuwepo mahakama ya juu, ambayo itafanya shuhuli zake vyema kwa vile hivi sasa kazi kubwa imekuwa ikifanywa na mahakama ya rufaa.
Nae mjumbe wa kamati namba 10, Dk. Kafumu, alisema wajumbe walio wengi wanapendekeza ibara hiyo ifutwe na badala yake wananchi waachwe kutuimia demokrasia yao.
Kuhusu elimu ya mgombea kuwa elimu ya kidato cha nne, alisema haipaswi kuwekwa ibara hiyo kwa kuwa hakuna nchi inayofuata kigenzi hicho na inaweza kuwanyima wananchi haki ya kumchagua mtu wamtakae.
Mjumbe Mahmoud Mussa Abdalla, akitoa maoni ya kamati yao namba 9, alisema suala la haki ya kupiga kura ya kumwajibisha Mbunge, wajumbe wa kamati hiyo walipendekeza ibara 129 ifutwe na kuandikwa upya, kwa kuzingatia nafasi ya mbunge ni ya muda maalum.
Alisema ibara mpya itaelekeza kwamba bunge litakuwa na mamlaka ya kutunga sheria itayoweza kuwawajibisha wabunge ambao wataonekana kushindwa kutekeleza wajibu wao.
Nae mjumbe Pindi Hadhara Chana, akitoa amaoni ya kamatu namba moja, alisema Makamu wa Pili wa Rais kama ataonekana kukiuka katiba, kamati yake imependekeza suala hilo lipelekwe bungeni na kama bunge litaridhia, maamuzi yatapelekwa Baraza la Wawakilishi, ambalo nalo likishindwa kumuwajibisha basi suala hilo litafikishwa mahakama ya katiba.
Hata hivyo, wajumbe wengine walipinga suala la uondoshwaji wa nafasi za wanawake kwa kupendekeza nafasi hizo sasa ziwe zinafanyika kwa wilaya.