Na Joseph Ngilisho, Arusha
RAIS Jakaya Kikwete,amesema serikali imepiga hatua katika kuboresha zana za ulinzi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na itaendelea kutenga fedha zaidi ili liweze kuwa na vifaa vya kisasa zaidi.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya kilele cha kuhitinisha zoezi la medali ya JWTZ,yaliyofanyika katika kijiji cha Nangururusu wilayani Monduli,ambapo maadhimisho hayo yalienda sambamba na maonesho ya zoezi la kivita kwa kutumia ndege, gari za deraya na jeshi la nchi kavu.
Alisema serikali imekuwa ikitenga fedha kila mwaka kwa lengo la kuboresha maslahi ya wanajeshi pamoja na kununulia vifaa vya kivita vinavyoendana na wakati ili jeshi hilo liendeleee kuimarika zaidi na kuweza kukabiliana na chokochoko zozote zinazoweza kujitokeza.
“Tunaendea kutenga fedha zaidi ili kuboresha maslahi ya wanajeshi,tuna mikakatia mingi ikiwemo ya kuwapatia nyumba, kujenga hospitali yao,tutaendea kufanya hivyo ili nitakapostaafu niliache jeshi likiwa katika hali nzuri kidogo,” alisema.
Aidha alisema tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo Septemba1964, halijawahi kuacha misingi iliyoasisiwa na mwalimu Julius Nyerere na kueleza kuwa litaendelea kusimamia misingi hiyo bila kukandamiza wananchi.
Naye Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussen Mwinyi, alisema pamoja na serikali kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa zana za kisasa,aliiomba iendelee kutenga fedha zaidi ili jeshi hilo likidhi mahitaji ya kuwa na vifaa vya kisasa zaidi.
“Amri jeshi mkuu ana wajibu wa kuangalia utendaji wa jeshi na vifaa vyake,hivyo tunaiomba serikali iendelee kutenga fedha zaidi ili zisaidie kununulia vifaa vya kisasa,” alisema.