Na Anna Nkinda,Maelezo
TAKWIMU zinaonesha idadi ya watoto wanaotumikishwa duniani inafikia milioni 169 kati ya hao wapo wenye umri wa miaka mitano, wanaotoka katika familia maskini ambao hulazimika kufanya kazi ili waweze kuishi na hivyo kukoa fursa ya upata elimu na malezi bora.
Kwa upande wa Tanzania asilimia 27.5 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 17 wanatumikishwa katika ajira hatarishi zikiwemo za kufanya kazi majumbani, sehemu za starehe, uvuvi, migodini, mashamba ya tumbaku na machungwa.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na mke wa Rais Kikwete, mama Salma Kikwete, wakati wa hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa ajili ya kampeni ya kupambana na utumikishwaji wa watoto iliyoandaliwa na International Rescue Committee (IRC) katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mama Salma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), alisema utumikishwaji wa mtoto ni hali inayomkosesha mtoto haki zake za msingi kama vile elimu, afya, malezi na kutopata nafasi ya kucheza na watoto wenzake.
“Utumikishwaji wa mtoto una madhara makubwa kwa mtoto mwenyewe, familia, jamii na taifa kwa ujumla. Kitendo hiki humsababishia mtoto kuathirika kiakili,kiafya kisaikolojia,kimakuzi na hata katika mazingira mengine hupelekea kifo chake,” alisema.
Pia husababisha umaskini kati ya kizazi hadi kizazi, na hivyo kudidimiza maendeleo ya taifa.
Aidha alisema mtoto anayetumikishwa hukosa ndoto za maisha bora kwa siku za usoni kwa kuwa alikosa fursa hiyo akiwa mdogo.
Alisema mazingira mazuri ya kisera na kisheria yametayarishwa kwa ajili ya kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji ukiwemo utumikishwaji katika ajira hatarishi na kinachotakiwa ni juhudi za pamoja ili kuhakikisha watoto hawatumikishwi.
Mkurugenzi wa IRC Tanzania, Elijah Okeyo, alisema ili kukabiliana na tatizo la ajira za watoto mwishoni mwa mwaka 2012 Serikali ya Marekani kupitia Idara ya Kazi iliwapatia dola milioni 10 kwa ajii ya mradi wa WEKEZA unaofanya kazi zake katika wilaya sita zilizopo mikoa ya Tanga na Kigoma.
Kupitia mradi huo, watoto 15,000 walitoka katika ajira hizo, walilindwa ili wasiweze kujihusisha na ajira za watoto na kuweza kurudi skuli kuendelea na masomo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa IRC wa kanda ya Afrika ya Mashariki na pembe ya Afrika, Kurt Tjossem, alisema kazi ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ni ya kila mtu na siyo ya mtu mmoja hivyo wadau wote wa watoto waendelee kuwekeza katika elimu kwani ndiyo ukombozi wa maisha yao.
Alisema inasikitisha kuona mtoto anaacha skuli na kwenda kufanya kazi ili aweze kuongeza kipato cha familia hali.