Na Mwandishi wetu
Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla, ametangaza nia ya kugombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao.
Kigwangalla anaungana na makada wengine, waliotangaza kugombea nafasi hiyo wakiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Hyyat Kilimanjaro jana akiwa ameambatana na mkewe na watoto wake pamoja na familia yake, alisema amefikia uamuzi huo bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu.
“ Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa kina; mahitaji ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto zangu, uwepo wa fursa ya kugombea na kushinda uchaguzi ujao, uwezo wangu wa kuchambua mambo, kutafakari, kufanya maamuzi sahihi, kuchukua hatua za utekelezaji na kusimamia utekelezaji, uadilifu na uzalendo wangu,” alisema.
Lakini zaidi alisema nia yake ya kuwa sehemu ya Watanzania wengi wanaotaka kuona mapinduzi ya kifikra ambayo yatakuwa chachu ya mabadiliko.
Alisema anatoa fursa Watanzania kumpima na kutizama mwenendo na uwezo wake na kwamba anaamini atapimwa na kuungwa mkono na ikitokea kutoungwa mkono hilo halitafanyika kwa misingi ya rangi ya ngozi yake, umri au dini.
Alisema Tanzania ina kila sababu ya kuwa dunia ya kwanza miaka 50 tokea kuungana na kwamba yuko tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala wasiwasi, kwa sababu wasipojitokeza watu kama yeye taifa litaongozwa na watu wasiostahiki.
“Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo na kesho; kupigana na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira kwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na umakini wa hali ya juu,” alisema.