Na Mwandishi wetu
Rais Jakaya Kikwete, leo anatarajiwa kukutana kwa mara ya pili wakuu wa vyama vya siasa vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kujaribu kukwamua mchakato wa katiba mpya.
Tayari Wenyeviti na Makatibu Wakuu kutoka vyama hivyo wapo mjini Dodoma kwa ajili ya kuendeleza mazungumzo hayo.
Kabla ya kukutana na Kikwete, viongozi hao wa TCD jana walikutana faragha ili kupata taarifa ya kamati iliyoundwa ambayo ilipewa jukumu la kuchambua na kutoa ushauri juu ya mambo watakayokwenda nayo katika mkutano huo.
Kamati iliyopewa jukumu hilo, inaongozwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia huku wajumbe wakiwa ni Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa na Katubu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kuweka msimamo wa pamoja kabla ya kukutana na Rais Kikwete.
Rais Kikwete anajaribu kukwamua mchakato wa katiba mpya, baada ya wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kususia bunge tokea mwezi Aprili, suala ambalo limezua mijadala mingi kuhusu uwezekano wa kupatikana katiba mpya.