Na Mwandishi wetu
Askofu Mkuu wa Kanisla la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe, amesema kinachoendelea katika Bunge Maalum la Katiba ni sawa na mchwa wanaotafuna fedha za Watanzania.
Alisema hayo jana katika mahubiri yake ya Jumapili katika kanisa lake liliopo Mwengee, Dar es Salaam.
Aidha alisema kanisa lake linaunga mkono tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu mchakato wa katiba.
Alisema kwamba Kanisa la FGBF linaunga mkono tamko hilo kwa asilimia 200.
"Tamko hili limekuwa likisomwa katika Makanisa ya Katoliki, KKKT, na mengineyo kuanzia Jumapili iliyopita, na leo (jana) nitalisoma kwenu, neno kwa neon,” alisema.
Alisema wakati umepita wa Wakristo kugawanywa, ili shetani atawale na kwamba tofauti zao wanazikweka pembeni na kuunganishwa na msalaba.
“Jukwaa la Wakristo Tanzania linawaunganisha wote wanaoamini juu ya msalaba - TEC, CPCT, CCT na SDA. Hivyo kauli ya Jukwaa la Wakristo Tanzania, ni kauli ya FGBF, kwa sababu sisi tuko ndani ya CPCT," Kakobe aliwaambia wafuasi wake.
Alisema rasimu ya pili ya Katiba ni waraka halali na rasmi, na ndiyo mawazo ya Watanzania na kuongeza kuwa katiba ni ya Wananchi na inahitaji maridhiano na sio ubabe.
Baada ya kusoma tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania la Agosti 28, 2014, aliwauliza waumini,"anayeunga mkono tamko hili asimame na kupunga mikono yake."
Ndipo wote kanisani waliposimama na kupunga mikono yao huku wakishangiria kasha Kakobe akasema:"Pamoja na umuhimu wa maombi, haitoshi tu kuomba; baada ya kufunga na kuomba, Esta alichukua hatua ya kumwambia ukweli Mfalme. Pamoja na maombi, hatua ya Jukwaa la Wakristo Tanzania kutoa sauti ya Kinabii kama hii, ni muhimu, ili mwenye masikio asikie."
Aliwataka waumini wake wawapuuze watu wanaosema kufanya hivyo ni kuchanganya dini na siasa.
“ Katiba siyo siasa, ni zaidi ya siasa;siasa imo ndani ya katiba, lakini ndani ya katiba kuna mambo mengi pia ambayo siyo siasa, kama vile dini, majeshi, mahakama, elimu, kilimo, ardhi, ufugaji, haki za binadamu,” alisema.