Na Aumbe Rashid
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum ya SMZ, Haji Omar Kheri, amewataka maofisa wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kuwa na umoja,upendo na ushirikiano na kuyatumia vyema mafunzo waliyoyapata kwa maslahi ya taifa.
Aliyasema hayo katika hafla fupi ya ufungaji wa mafunzo ya kozi ya Platuni Kamanda,iliyofanyika kikosi cha JKU Kama wilaya ya magharibi Unguja.
Aliwataka wahitimu wa mafunzo hao kuzingatia majukumu yao, wanaporejea katika vituo vyao vya kazi.
Alisema ushirikiano ndio silaha ya shinda changamoto zote zinazolikabili jeshi hilo.
Aliwaasa kutokuwa chanzo cha migogoro kwa sababu inaweza kuchafua jeshi badala yake wafanye kazi kwa busara zaidi.
Aliwataka wakuu wa idara za jeshi hilo kusimamia vyema majukumu yao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Mkuu wa JKU, Kanali Soud Haji Khatib, aliwapongeza wahitimu na wale wote waliosaidia kufanikisha mafunzo hayo,wakiwemo walimu kutoka Jeshi la Kujenga Tafa (JKT) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ).
Wahitimu katika risala yao walisema wanakabiliwa na upungufu wa madarasa ya kusomea, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha askari 37 wakiwemo wanawake saba.