Na Laylat Khalfan
TANI 14.35 za majongoo ya pwani, zimesafirishwa nje ya nchi kwa mwaka 2013.
Akizungumza na mwandishi wa habari ofisini kwake Maruhubi, Mkuu wa kitengo cha usarifu na ukuzaji wa masoko,Hamad Khatib, alisema kiwango hicho kimeshuka ikilinganishwa na tani 21 zilizosafirishwa mwaka 2012.
Alisema sababu za kupungua usafirishaji majongoo ni upungufu wa mazao hayo kutokana na kuongezeka idadi ya wavuvi.
Alisema soko kubwa la majongoo ya Zanzibar ni Marekani,Korea, Honkong, Vietnam, Dubai na nchi nyengine za Ulaya.
Kwa upande wake, Hashim Muumin ambae ni Mtafiti wa mazao ya baharini, alisema majongoo yapo hatarini kutoweka kutokana na kuongezeka idadi ya wavuvi.
Aidha alisema ipo haja kwa serikali kuweka mikakati madhubuti ili kuunusuru uvuvi huo.
Hata hivyo, alisema wameandaa mikakati ya kuzalisha vifanga vya majongoo na baadae kuyaweka katika sehemu yaliyopungua.