Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Wenye ulemavu wawasilisha tena maoni bunge la katiba

$
0
0
Na Benedict Liwenga, Maelezo
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amewahakikishia watu wenye ulemavu nchini kuwa wanatendewa haki katika katiba mpya itakayopatikana.

Aliyasema hayo jana katika mkutano wake na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), ambao walifika bungeni kwa lengo la kuwasilisha hoja zenye msisitizo kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika mchakato wa katiba.

Alisema makundi yanayofika bungeni, hayaendi na hoja mpya bali ni mawasiliano ya kawaida yanayohusu safari kutoka rasimu ya katiba mpaka kufikia katiba mpya.

“Jambo lolote lililoandikwa na binadamu halikosi kasoro, katika rasimu hii ya katiba tumegundua mapungufu kadha,kuna baadhi ya maoni ambayo hayakuzingatiwa ndiyo maana tunayafanyia kazi ili yawemo katika katiba mpya,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inclusive Development Promoters and Consultants kutoka  Dar es Salaam, Kaganzi Rutachwamagyo, ambaye pia ni mwanachama wa shirikisho hilo,alisema kikosi cha ushauri kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu kimeweka kipaumbele cha msisitizo wao ambao unajielekeza katika hoja za kuongeza masuala ya mambo ya Muungano.


Alisema hoja nyingine ya msisitizo inahusiana na uanzishwaji wa chombo cha uratibu wa haki, usawa wa fursa na uwajibikaji wa haki za watu wenye ulemavu.

Aligusia pia juu ya hoja nyingine inayohusu suala la uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwenye Bunge,Baraza la Wawakilishi na  mabaraza ya Madiwani.

“Mathalani, tunapendekeza kifungu 113 kisomeke kuwa asilimia 5 ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakuwa ni watu wenye ulemavu wakiwakilisha kundi hili na watapatikana kwa kuchaguliwa na wahusika wenyewe,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu, Amon Mpanjo, ambaye ni mjumbe wa bunge hilo alimuomba Mwenyekiti wa bunge maalum kuunga mkono sio kupokea maoni mapya, bali kuyaboresha yale yaliyokwisha wasilishwa hapo awali.


“Tukuombe Mwenyekiti ulisisitizie bunge letu maalum la katiba liweze kuzingatia haki za watu wenye ulemavu ili nao wapate kuwa na maisha bora,” alisema.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>