Na Mwantanga Ame
WAKATI mbio za urais wa Tanzania zikianza, mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi, amesema Rais mpya anatakiwa awe mtu mwenye sifa wa kuwatumikia Watanzania na sio mbaguzi wa kidini.
Aliyasema hayo wakati akiwahutubia wanachama wa CCM katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Chiuyu, wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida.
Alisema baadhi ya wanaotaka urais wanapita kwa wananchi wakiwambia Rais ajae lazima awe Mkiristo wa madhehebu ya Roman jambo ambalo ni hatari.
Alisema makundi hayo yameanza kujenga dhana za udini, ukabila na umajimbo, mambo ambayo ni hatari.
Alisema hiyo ni hatari kubwa na ndio maana Rais wa kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, alikemea ubaguzi na udini.
“Kuna wenzetu wanataka kutuletea ubaguzi, watuletee nakama, watuletee balaa kwa hivyo tutahadhari na watu wa aina hiyo,ukija uchaguzi tusizungumze habari ya ukabila wala udini awe Mkiristo au Muislamu,” alisema.
“Sasa hao wanaotembeza vikaratasi tuwe na tahadhari nao kwa sababu nchi nyingi zimepata nakama kwa sababu ya ubaguzi wa ukabila na ubaguzi wa kidini,” alisema.
Alisema atahakikisha anasimamia kazi kubwa iliyoanzishwa na chama ili kiweze kushika dola katika uchaguzi mkuu ujao.