Na Hafsa Golo
JUMLA ya watoto 5,030 wameokolewa katika ajira mbaya na kurejeshwa skuli katika maeneo tofauti Unguja na Pemba.
Aidha familia 920 zimeanzishiwa miradi mbali mbali ili kuwaendeleza watoto wao kielimu.
Ofisa usimamizi wa mradi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Sheikha Haji Dau,alisema hayo katika ziara maalum ya kuangalia mwenendo wa watoto hao kwa baadhi ya skuli wanazosoma.
Alisema watoto hao wana umri chini ya miaka 18 na tayari walikuwa wameacha masomo na kujishughulisha na ajira mbaya na wengine walikuwa kwenye hatari ya kuingia katika ajira hizo.
Alisema watoto hao wametoka katika shehia 45 za Unguja na Pemba na miongoni mwa kazi walizokuwa wakizifanya ni pamoja na kuvunja kokoto,kupara samaki na kuvua,kukokota magari ya ngombe na kufanyakazi mahotelini.
Akizungumzia familia za watoto masikini zaidi walioanzishiwa miradi, alisema lengo la kuanzisha miradi hiyo ni kuhakikisha watoto hao wanapata haki ya msingi ya elimu.
Khalfan Abdalla (13) mkaazi wa Pwani Mchangani ambae miongoni mwa wanafunzi waliookolewa katika ajira mbaya, aliliambia Zanzibar Leo kwamba kutokana na ugumu wa maisha alilazimika kujishughilisha na kazi ya kupara samaki ili kupata fedha za kusaidia familia yake.
“Nyumbani naishi na bibi,nilikuwa nikienda Matemwe kupara samaki nikurudi nampa pesa bibi na kwa siku napara samaki 30 hadi 40 na kuna siku nilichomwa na mwiba wa tasi nikaumia sana nikajishughulisha na kazi ya nyengine,” alisema.
Nae Siliji Hamad Juma, alisema mpango wa miradi kwa familia maskini umeweza kuwapunguzia ukali wa maisha na kusaidia watoto wao kurejea skuli.
Mradi wa ajira za watoto unatekelezwa na Mfuko wa Hifadhi ya Mtoto (Save the Children), Jumuia ya Kuharakisha Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (COWPZ),Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Jumuia ya Kupunguza Umasikini na Kuboresha hali za Wananchi kisiwani Pemba (KUKHAWA ) na Jumuia ya Kupambana na Umasikini kisiwani Pemba, (PIRO) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).