Na Fatina Mathias, Dodoma
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinachoundwa na vyama vya siasa, kimekubali mjadala wa Bunge la Katiba uendelee hadi Oktoba 4, ndipo Bunge hilo liahirishwe.
Tamko hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo wakati akizungumza na waandishi wa habari bungeni mjini Dodoma.
Alisema bunge hilo kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa tangazo la serikali namba 254 lililotolewa na Rais Jakaya Kikwete.
“Kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba baada ya bunge hilo kumaliza kutunga katiba,ingefuata hatua ya kura ya maoni kuthibitisha katiba hatua ambayo italazimisha uchaguzi mkuu wa 2015 kuahirishwa, hivyo tumeona ni kheri mchakato uahirishwe na uendelee baada ya uchaguzi mkuu wa mwakani,”alisema.
Alisema pamoja na kazi inayofanywa na bunge hilo, lakini haliwezi utoa katiba mpya itakayotumika katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa muda hautoshi kukamilisha kazi hiyo.
Aidha alisema kwa mujibu wa sheria ya mabadiliko ya katiba mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika mwezi Aprili mwakani na kama itabidi kurudiwa kwa mujibu wa sheria iliyotajwa itabidi irudiwe mwezi Juni au Julai 2015 muda ambao bunge la Jamhuri linatakiwa livunjwe kwa ajili ya uchaguzi mkuu, hivyo ili katiba mpya itumike kwenye uchaguzi inabidi uhai wa bunge uongezwe zaidi ya 2015 jambo ambalo hawaliungi mkono.
Alisema kwa sasa inabidi matayarisho kwa ajili ya uchaguzi wa vijiji,vitongoji na mitaa yaanze haraka iwezekanavyo kwa serikali kuchukua hatua za kisheria ili uchaguzi ufanyike mapema mwakani.
“Kwamba kwa vile uchaguzi mkuu utafanyika kwa kutumia katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 ni muhimu kufanya mabadiliko kidogo katika katiba pamoja na sheria ya uchaguzi itakayowezesha nchi kufanya uchaguzi huru na wa haki,”alisema.
Alitaja mambo ambayo wameyakubali kuwa ni kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi ambayo itasimamia uchaguzi na mshindi wa uchaguzi wa rais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50.
Alisema viongozi wakuu wa vyama wanaounda TCD wamempongeza Rais Kikwete kwa ujasiri wake na imani yake katika kuimarisha demokrasia nchini wa kuanzisha mchakato wa kuandika katiba ya nchi.
Aidha walimpongeza Rais kwa kukubali kukutana na kushauriana kuhusu mambo ya muhimu kwa mustakabali wa Taifa kwa lengo la kudumisha amani,upendo na mshikamano.
Vyama vinavyounda TCD ni CCM, CHADEMA, CUF, NCCR MAGEUZI, TLP, UDP ambavyo vina wawakilishi bungeni na UPDP kinachowakilisha vyama visivyo na wabunge bungeni.