Na Joseph Ngilisho,Arusha
Mtoto Lowasa Ingine (15), mkazi wa kijiji cha Sepeto, wilayani Monduli,amelazwa hospitali ya Seliana, iliopo mjini Arusha, baada ya kujeruhiwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu kwenye mikono yake miwili.
Akizungumza kwa shida katika hospitali hiyo, alisema siku ya tukio Septemba 7 mwaka huu, majira ya saa 8:00 mchana alikuwa kwenye eneo la jeshi ambalo lilitumika kufanyia mazoezi ya kivita Septemba 5 mwaka huu kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya jeshi hilo.
Alisema wakati akiwa eneo hilo kwa ajili ya kuchunga ng’ombe yeye na wenzake waliokota kitu kinachofanana na chuma.
“Nilipookota nilikuwa na wenzangu, wakati nikikiangalia na huku nikijaribu kufungua,ghafla nikasikia kishindo na kikaanguka chini na kupoteza fahamu,”alisema.
Alisema baada ya kushituka alijikuta yupo hospitalini na tayari kiganja chake cha mkono wa kulia na mkono wa kushoto kimekatwa vidole vinne na kubakiwa na kidole kimoja.
Kaka wa mtoto huyo,, Miage Ingine, alisema mdogo wake alikwenda eneo la jeshi kuchunga ng’ombe akiwa na wenzake watatu, akiwa huko ng’ombe alikanyaga kitu ambacho kiliripuka na kumkata mdogo wake mikono na ng’ombe kukatika miguu.
“Baada ya tukio hilo tulipata taarifa kutoka kwa majirani zetu na tukaenda kuwachukua ambapo tuliwapeleka hospitali ya wilaya Monduli ambako walihudumiwa na wenzake kwa kuwa hawakuumia sana waliruhusiwa ila mdogo wangu aliyekatwa vidole na kiganja tuliamuriwa tuje Selian,”alisema.
Alisema baada ya tukio hilo walitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kijiji chao, ambaye aliahidi kupeleka taarifa jeshini.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Geofrey Kichira, alithibitisha kumpokea mtoto huyo akiwa amepoteza kiganja na vidole tisa.
“Mtoto huyu tumempokea na tunaendelea kumpatia huduma na hali yake inaendelea vizuri tofauti na alipofika,”alisema.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa JWTZ, Kanali Erick Komba, akizungumza kwa njia ya simu, alisema jeshi halina taarifa na tukio hilo na wanalifuatilia.