Na Mwandishi wetu,Dodoma
Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Maalum la Katiba ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu, wametaka suala la mahakama ya kadhi iingizwe kwenye katiba mpya.
Mvutano huo ulijitokeza jana wakati wakichangia mjadala wa rasimu ya katiba baada ya kamati 12 za bunge hilo kumaliza kuwasilisha taarifa za mapendekezo yao.
Mmoja wa wajumbe hao, Shekh Hamid Jongo, aliitaka katiba itamke kwamba kutatungwa sheria ambayo itaeleza kwamba masuala ya ndoa, mirathi na talaka yataamuliwa kwa mujibu wa imani ya dini ya kiislamu.
Alisema katika sura ya 10 ibara ya 150 (3) ya rasimu ya mabadiliko ya katiba inaleza kwamba mahakama ndio chombo cha mwisho cha kutoa haki na katika dini ya kiislamu mambo ya ndoa, mirathi, wakfu na talaka yanaamuliwa kidini, hivyo utoaji haki kwa mambo hayo ni ibada.
Aidha alisema kutambulika kwa mahakama ya kadhi kisheria hakuzuii watu wa madhehebu mengine na wao kudai mambo wanayoyataka kuwemo katika katiba.
“Waislamu mambo ya mirathi, talaka, ndoa ni ibada yetu na kamba yanakataliwa kuamuliwa katika mahakama ya kadhi,” alisema.
Naye mjumbe mwingine,Dk. Zainab Gama, alisema umefika wakati sasa kilio cha Waisalamu cha kutaka mahakama ya Kadhi kutambulika kisheria kisikilizwe ili kunusuru amani iliyopo.
“Chonde chonde nchi yetu hii ina amani tusiruhusu watu kutumia udhaifu ulipo kuvunja sheria, pamoja na kwamba Waislamu wameruhusiwa kuanzisha mahakama za kadhi lakini mahakama hizi hazitambuliki kisheria,”alisema.
Alisema mambo yanayoamuliwa na mahakama za kadhi yanapofikishwa katikamahakama za kawaida hutupiliwa mbali.
Kwa upande wake, Shamimu Khan, yeye alitaka kujua kigugumizi kiko wapi kutokana na kushindwa kuingiza mahakama ya kadhi katika katiba na sheria za nchi.
Alisema kilichopo sasa Waislamu wanapigwa danadana kwamba suala la mahakama ya kadhi litawekwa kwenye sheria na kusema jambo hilo haliwezekani kama limeshindwa kutambulika katika sheria mama ambayo ni katiba.
Mbwana Salum Mbanda yeye alitaka mahakama ya kadhi itambuliwe kikatiba na Serikali igharamie katika uendeshaji wake.
Mjumbe mwingine, Hamisi Ally Togwa, alisema pamoja na ibara ya 32 ya katiba kueleza uwepo wa uhuru wa imani ya kuabudu dini yoyote lakini Waislamu wamekuwa wakiikosa haki hiyo kwa muda mrefu.
Baada ya kuchangia, suala hilo liliibua mvutano ambapo baadhi ya wajumbe walipinga mahakama hiyo kutambulika kikatiba akiwemo Ave Maria Semakafu na Jasson Rweikiza.
Rweikiza alisema ni makosa kwa Katiba kuzungumzia mahakama ya kadhi wakati serikali haina dini.
Suala jingine lililoibuka ni uraia pacha ambapo baadhi ya wajumbe walipendekeza uraia pacha uruhusiwe kikatiba.
Aliyekuwa wa kwanza kuunga mkono uraia pacha ni Mbunge wa kuteuliwa na Rais, Zakia Meghji ambaye alisema Watanzania wenye uraia wa nchi za nje, walilazimika kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali.
Mapendekezo hayo ya Meghji yaliungwa mkono na mjumbe mwingine ambaye ni Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), aliesema suala la uraia pacha halipaswi kupigwa vita kwa kuwa ni jambo la kawaida duniani na kwamba Watanzania wenye uraia wa nchi za nje, walifanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali.