Na Ramadhani Ali, Melezo
Mkurugenzi wa Idara ya hospitali za Mnazimmoja,Dk. Jamala Adam Taib, amesema kazi kubwa inayofanywa na idara hiyo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2010 ni kuimarisha hospitali ya Mnazimmoja ifikie kiwango cha hospitali ya rufaa.
Alisema hatua zinazochukuliwa na idara ni kuimarisha miundombinu, kusomesha wataalamu wa fani tofauti za afya, kuimarisha uchunguzi wa maradhi na kuhakikisha dawa zinapatikana.
Alimueleza Waziri mpya wa Afya, Rashid Seif Suleiman, alipofanya ziara ya kutembelea hospitali hiyo kuangalia utendaji wa kazi na changamoto zinazoikabili.
Alisemamajukumu yote waliyopangiwa katika kuimarisha hospitali kuu ya Mnazimmoja yamefikia hatua nzuri na hivi sasa wananchi wamejenga matumaini makubwa kutokana na huduma zake.
Alisema idara ya hospitali za Mnazimmoja ina wafanyakazi 800 wakiwemo madaktari bingwa 14 na serikali inaendelea kusomesha wataalamu wa fani mbali mbali ambapo wanafunzi 200 wa fani ya udaktari wapo vyuoni.
Pamoja na mafanikio makubwa yaliyofikiwa na hospitali kuu ya Mnazimmoja, alisema bado inakabiliwa na ufinyu wa bajeti na mageuzi.
Msaidizi Mganga Mkuu wa hospitali kuu ya Mnazimmoja, Dk. Muhidini Abdalla Mohamed. amemueleza Waziri wa Afya ambae alifuatana na Naibu wake, Mahmoud Thabit Kombo, kwamba kliniki ya meno ya hospitali hiyo ina vifaa vya kisasa kutoka shirika la MCW la Marekani na kuifanya kuwa kliniki bora zaidi kuliko hospitali nyengine za Zanzibar.
Aliwahakikishia wananchi kwamba huduma za matatizo yote ya meno zinapatikana kwenye kliniki hiyo na kuwataka wananchi kutokuwa na wasi wasi na waendelee kuitumia.
Katika kitengo cha maradhi ya kisukari, Daktari Msaidizi wa maradhi hayo,Miskia Ali Mohammed alimueleza Waziri kwamba maradhi hayo yanaongezeka kwa kasi na kumekuwa na upungufu mkubwa wa dawa.
Alisema tatizo jengine linalokikabili kitengo hicho ni upungufu wa chakula cha wagonjwa wa kisukari wanaolazwa ambacho kinatakiwa kiliwe sambamba na matatibabu wanayopatiwa ili dawa wanazotumia zifanye kazi kwa ufanisi.
Waziri wa Afya kwa upande wake aliwataka viongozi wa idara hiyo kuimarisha umoja na mshikamano na watendaji wao ili kufanikisha malengo yaliyoweka ya kuwahudumia wananchi na kuwapa huduma nzuri.