Na Haroub Hussein, Dar es Salaam
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa taasisi za kodi Afrika.
Mkutano huo utakaoanza tarehe 15 hadi 19 mwezi huu utafunguliwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari maelezo jijini hapa, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, alisema Tanzania imepata fursa kwa mara ya kwanza kuandaa mkutano huo muhimu kwa taasisi za kodi ambapo utakua mkutano wa tatu tangu kuanzishwa kwa taasisi za kodi Afrika (ATAF) mwaka 2009.
Alisema lengo la mkutano huo ni kujadili namna ya kuimarisha taasisi za kodi Afrika, kujenga uwezo wa watumishi katika taasisi za kodi, kubadilishana uzoefu wa ukusanyaji wa kodi katika sekta mbali mbali pamoja na kubadilishana taarifa muhimu za biashara za kimataifa na uwekezaji katika nchi za Afrika.
Aidha alisema mkutano huo utawakutanisha wakuu wa mamlaka za mapato, wataalamu wa masuala ya kodi kutoka mataifa 37 ya Afrika ambao ni wanachama wa ATAF pamoja na wafadhili ambapo watajadili masuala mbali mbali ya kodi katika bara la Afrika pamoja na kuchagua baraza jipya la ATAF.
Alisema mada mbali mbali zitajadiliwa katika mkutano huo ikiwa pamoja na uongozi katika ajenda ya kodi kimataifa, kuzingatia weledi, kanuni na misingi bora ya uongozi na utawala, usimamizi wa rasilimali watu, usawa wa jinsia katika mafanikio ya makampuni, taswira za kodi Afrika pamoja na kuunda fursa za baadae kwa Afrika katika kodi za kimataifa.
Alisema mbali na washiriki wa mkutano huo kujadili masuala ya kodi pia watapata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni ‘Tathmini ya Uongozi na mikakati ya usimamizi wa ajenda ya kodi Afrika.’