STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Septemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia umeiwezesha Zanzibar kufaidika na misaada mbali mbali ya kimaendeleo inayotolewa na benki hiyo kwa nchi wanachama.
Akizungumza na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Benki hiyo Sri Mulyani Indrawati ofisini kwake Ikulu leo, Dk. Shein amesema amefurahishwa na namna ya utayari wa Benki hiyo wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki hiyo ni wa muda mrefu na kwamba si rahisi kueleza kila mchango wa benki hiyo kwa maendeleo ya Zanzibar.
Kwa hivyo Dk. Shein aliishukuru Benki ya Dunia kwa misaada yake hiyo kwa Zanzibar ambayo aliielezea kuwa imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Zanzibar na kuinua hali za maisha za wananchi wake.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameitaja baadhi ya miradi mikubwa ambayo benki hiyo inasaidia Zanzibar kuwa ni pamoja na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Mradi wa kuimarisha huduma katika mji wa Zanzibar, Mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Maeneo ya Bahari pamoja na sekta ya elimu chini ya Mpango wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari Zanzibar.
Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi Mtendaji huyo kuwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume utaimarisha uchumi wa Zanzibar kwa kuwa ufanisi wake utarahisisha wageni wengi kuingia nchini hivyo kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar.
Alibainisha kuwa mpango wa Serikali ni kuangalia namna ya kuiunganisha sekta ya utalii na sekta nyingine ambapo kwa kufanya hivyo itaweza kutoa ajira nyingi kwa wananchi wa Zanzibar.
Kuhusu suala zima la kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini Dk. Shein alimueleza Sri Indrawati kuwa Serikali imeandaa mkakati maalum ambao unafanyiwa kazi hivi sasa.
Aliongeza kuwa msaada ya Benki hiyo katika kuimarisha elimu ya sekondari umetoa matokeo mazuri ambapo imeiwezesha Zanzibar kuwa na miundombinu bora ya elimu lakini changamoto kubwa inayoikabili sekta hiyo sasa ni suala la ubora wa elimu hasa katika masomo ya sayansi ambapo kuna uhaba mkubwa wa walimu wa masomo hayo.
Dk. Shein alimueleza Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunuia kuwa pamoja na misaada iliyokwishatolewa na Benki hiyo lakini ni dhahiri ushirikiano zaidi kutoka benki hiyo unahitajika ili kusaidia Zanzibar kufikia malengo ya Dira ya maendeleo 2020, pamoja na Mkakati wa Kupunguza Umasikni na Kukuza Uchumi-MKUKUTA.
Kwa hivyo alisema ana matumaini makubwa kuwa Benki hiyo itaendelea kushiriana na Zanzibar katika awamu nyingine ya kuimarisha mindombinu ikiwemo ya barabara za kuunganisha mji wa Zanzibar ambapo uchambuzi yakinifu kwa barabara ulikwishafanyika kwa msaada wa benki hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu huyo Sri Mulyani Indrawati alimhakikishia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa Benki ya Dunia iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kufikia malengo ya mipango yake mbali mbali ya maendeleo.
Alimueleza Mhe Rais kuwa uongozi wa Benki yake umefurahishwa na namna inavyopata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutekeleza programu mbalimbali.
Alifafanua kuwa ziara yake Zanzibar imelenga katika kuimarisha ushirikiano kati Benki ya Dunia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuangalia namna ya kuendeleza kutekeleza ahadi za benki hiyo katika kufikia malengo ya mipango ya maendeleo ya Zanzibar ukiwemo MKUKUTA.
Sri Mulyani Indrawati alibainisha kuwa ni dhamira ya benki hiyo kuona Zanzibar inafanikiwa kuondosha umasikini na kuimarisha ustawi wa maisha ya wananchi wake kwa kuongeza ajira zenye kipato kizuri ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta binafsi sambamba na kuifanya sekta ya utalii kutoa ajira za nyingi na za uhakika.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na baadhi ya Mawaziri na Makatibu wa wakuu pamoja na watendaji wengine wa Benki ya Dunia akiwemo Mwakilishi wa Benki hiyo katika nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bwana Philippe Dongier.