Na Hafsa Golo
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Juma Ali Juma, amesema Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuinua uchumi na kipato cha wananchi kupitia zao la karafuu.
Aliyasema hayo jana ofisi kwake Darajani wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema karafuu zinaweza kupunguza kiwango cha umaskini iwapo zao hilo litaimarishwa.
Alisema serikali inaendelea kutoa msukumo kuimarisha zao hilo ikiwemo kuwapa wakulima asilimia 80 ya bei katika soko la dunia.
‘
Aidha alisema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali kupitia wizara hiyo ni kuhakikisha wakulima wanapatiwa miche ya mikarafuu ili kuuimarisha kilimo hicho.
Alisema mkulima hupatiwa miche 40 ya mikarafuu lakini kiwango hicho huongezwa baada ya kuthibitishwa mkulima na uwezo na eneo la kuipanda.
Alisema katika msimu wa mwaka 2014 wizara imeotesha miche 1,000,000 ya mikarafuu kati ya hiyo 503,560 imefikia umri wa kupandwa.
Alisema miche 178,540 tayari imepandwa Unguja na miche 325,020 imepandwa Pemba.
Alisema miongoni mwa changamoto zinazojitokeza katika uimarishaji wa zao hilo ni pamoja na ukataji wa miche ya zao hilo na kurejesha nyuma juhudi za wakulima.