1. Mwandishi Yussuf Shoka Hamad (kulia) akiwa na Professa Said Ahmed Muhamed ali[omtembelea nyumbani kwake Limbani Wete hivi karibuni.
Na: Ali Othman Ali
Mwandishi anayechipukia kwa kasi katika tasnia ya fasihi ya Kiswahili ambaye pia ni Mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu Cha London, SOAS na Cambridge nchini Uingereza, Bwana Yussuf Shoka Hamad, hivi karibuni anatarajia kutoa kitabu chake kipya na cha kwanza kuchapishwa kinachoitwa; ‘Paka wa Binti Hatibu na Hadithi Nyingine’.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa simu kutoka nyumbani kwake jijini London, Bwana Yussuf alisema; ‘ Msomi kama binadamu hufa, huzikwa na husahaulika kama watu wengine wengi. Lakini msomi kama mwanataaluma na mwandishi hafi, hazikwi, na wala hawezi kusahaulika kwani mawazo, fikra na falsafa zake hubakia katika maandishi anayoyaacha. Na maaandishi hayo huwa ukumbusho na urithi auachiyao jamii yake milele na milele.’
Bwana Yussuf pia alifafanua kwa upana kwanini ameamua kuandika kitabu chake kwa kutumia lugha ya Kiswahili kwa kusema kwamba hadithi zilizomo humo zinawalenga waswahili wenyewe na sio watu wa jamii nyengine. Kwa hivyo, sambamba na kukuza na kukitangaza Kiswahili kimataifa, kitabu hicho kitatumika kuufiskisha ujumbe uliokusudiwa kwa jamii kwa urahisi na kwa wepesi kwani lugha iliyotumika ni nyepesi na yenye kufahamika kwa walengwa.
Alipoulizwa kwanini alichagua kukipa kitabu chake hicho jina la ‘Paka wa Bini Hatibu’ mwandishi alisema; ‘ Paka wa Binti Hatibu ni usemi uliozoeleka na wengi. Ingawa kufahamika kwake kimaana na kimantiki kumekuwa kukileta mashaka yatokanayo na bezo, kebehi na dharau, usemi huu unabaki kuwa na maana pana, tena zaidi ya ile iliyozoeleka kimazowea ya kuukamilisha usemi wenyewe. Jina la Paka wa Binti Hatibu, halimmuliki paka kama paka peke yake na Binti Hatibu kama tumjuavyo, bali kinaimuilika jamii yote na wanajamii, wote kwa ujumla.’
Akitoa ufafanuzi kuhusu kitabu chake hicho ambacho utangulizi wake umeandikwa na Mhadhiri wa masomo ya Fasihi wa Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) Bi Asha Khamis Hamad, mwandishi huyo alisema kitabu chake kina hadithi saba na kila hadithi kama kawaida yake ina ncha nyengine saba zinazoimulika jamii kwa undani na kwa kina kipevu cha udadisi na upekuzi. Kila hadithi imebeba mikasa, vitimbi na viteweji kedekede ambavyo kwa ujumla hutoa ujumbe na kuleta ladha ya ucheshi usio kikomo.
Akijibu suala la vipi na wapi aliuota ujuzi huo wa uandishi, mwandishi alisema kuwa. Amekuwa akisoma kazi mbali mbali za waandishi, na pia ametembea sana na kusikia mengi kutoka kwa magwiji wa simulizi na uandishi wakiwemo waandishi nguli katika fasihi ya Kiswahili kama vile Professa Said Ahmed, Farouk Topan na Ali Mwalimu Rashid ambao kwa pamoja walimpa moyo na ari ya kuandika.
Kitabu cha Paka wa Binti hatibu kinachapishwa na ‘The Jomo Kenyatta Foundation’ ya Nairobi nchini Kenya na kitatumika kama kitabu cha kiada katika masomo ya Fasihi katika chuo kikuu cha London, SOAS nchini Uingereza mara tu baada ya kutoka hivi karibuni.
Mbali na kitabu hiki, mwandishi huyu pia amekamilisha miswada mengine minne ya riwaya na Hadithi fupi zinazosubiri kuchapishwa. Mwandihi hivi sasa anaandika vitabu vya kitaaluma vya kufundishia Kiswahili shuleni na vitabu vitokanavyo na utafiti wa mambo mbali mbali yahusuyo jamii na utamaduni wa watu wa Pemba. Moja ya muswada wa kitabu kitokanacho na utafiti wake ni kile cha ‘Watu 40 Mashuhuri kutoka Pemba’ ambacho utafiti wake unaendelea hivi sasa.