Na Mwantanga Ame
SERIKALI imesema hakuna mgogoro wa kisiasa na kisheria Tanzania na haiko tayari kuruhusu kundi lolote kuvunja sheria za nchi.
Tamko hilo limetolewa mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe.Dk. Asha Rose Migiro, wakati akiwasilisha tamko hilo kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Tamko hilo inakuja wakati CHADEMA ikipanga kuitisha maandamano na migomo ya nchi nzima kupinga kuendelea mchakato wa katiba.
Alisema wito unaotolewa na baadhi ya viongozi wa kulazimisha kusitisha bunge hilo sio sahihi kwani taifa halina mgogoro wa kisiasa na serikali itahakikisha hakuna mtu atakaevuruga amani iliyopo.
“Hakuna sababu ya kuruhusu watu kujazwa hofu, serikali ipo macho na itasimamia sheria na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kutafuta riziki na mchakato huu upo kisheria,” alisema.
Aidha alisema mahakama kuu imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa kutaka bunge hilo lisitishwe.
Alisema uamuzi huo wa mahakama, unathibitisha bunge hilo lipo kihalali.
Alisema hadi juzi usiku wakati bunge hilo linafanyiwa uhakiki kulikuwa na wajumbe 500 sawa na asilimia 79 ya wajumbe wote 630, wakati wabunge waliosusia kuingia ni 130.
Alisema kundi la 201 lina wajumbe 189 wanaoshiriki bunge hilo jambo ambalo linaonesha wazi kuwa idadi hiyo haina kikwazo kwa shughuli za bunge.
Alisema wajumbe 348 wanaotoka Tanzania Bara kati yao 125 wanatoka kundi la 201 na kwa wajumbe wanaotoka Zanzibar wapo 152 ambapo kati yao 64 ni wa kundi la 201.
Alisema bunge hilo, lina wawakilishi wanaotoka vyama 18 vya siasa wakati vyama vilivyosusia ni Chadema, CUF na NCCR Mageuzi.