Na Mahmoud Ahmad
Halmashauri ya jiji la Arusha ipo mbioni kukifanya kituo cha afya cha Lovolosi kuwa hospitali ya jiji kwa kupanua majengo yake na kuweka vifaa tiba vya kisasa lengo likiwa kuwapatia huduma bora za afya wakazi wa jiji hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Juma Iddy, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuelezea mikakati ya kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.
Alisema hatua hiyo inakuja baada ya jiji kufungua kituo cha afya cha daraja mbili chenye uwezo wa kutoa huduma kwa wakazi zaidi ya 19,000 wa kata za Daraja Mbili,Sokon 1,Lemara na maeneo ya jirani kituo kilichozinduliwa na mwenge wa uhuru.
Alisema mpango wa uboreshaji wa kituo cha afya Levolosi kuwa hospitali ya jiji umeshaanza ambapo fedha za mradi huo wa upanuzi na uwekaji wa vifaa tiba vya kisasa zinatolewa na halmashauri ya jiji Arusha.
Akizungumzia sekta ya elimu alisema jiji limeongeza vyumba vya madarasa na kujenga maabara za kisasa kwenye skuli za sekondari za kata ikiwemo pia kuongeza madawati lengo likiwa wanafunzi kupata elimu bora na kuondokana na tatizo la wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kukosa vyumba vya madarasa.
Alisema mpango huo umeshaanza kwenye skuli za Sonrenyi, Naura, Engutoto,Ngarenaro na Felex Mrema na kwamba kwa sasa wamebakiza vyumba vya madarasa tisa tu hadi mwisho mwa mwezi huu watakuwa wameshakamilisha madarasa hayo.
Aidha alisema halmashauri ya jiji la Arusha imenunua vifaa vya ujenzi wa barabara yakiwemo magari matatu,greda na kijiko vitakavyotumika katika ujenzi na ukarabati wa barabara za jiji wakati pia magari yatasaidia uzoaji taka katika maeneo jiji.
Alisema jiji limejitahidi kuboresha madaraja na barabara zake na ipo mbioni kujenga barabara ya Unga Ltd hadi Terati yenye urefu wa kilometa saba kwa kiwango cha lami ambapo fedha zake zimepatikana na mradi huo kukamilika ndani ya miezi 14.