Na Khamisuu Abdallah
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Islam Seif, amesema miongoni mwa mikakati iliyowekwa na ofisi hiyo katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kupanda miti pembezoni mwa bahari na juu Unguja na Pemba.
Alisema hayo katika hafla ya upandaji miti katika kijiji cha Fuoni Kibondeni.
Nae Mkuu wa wilaya ya magharibi Unguja, Ayoub Mohammed aliishauri jamii uwa mstari wa mbele kuwadhibiti wanaoharibu mazingira na kuwahamasisha kupanda miti ili uoto wa asili uendelee kuwepo.
Alisema ili kuyahifadhi mazingira na kuyakinga maji ya bahari yasivamie vijiji ni vyema kuwafichua watu hao na kuhakikisha rasilimali hiyo inalindwa kwa hali na mali.
Alisema Zanzibar ni moja ya kisiwa kidogo kilichozungukwa na bahari hivyo kuharibu mazingira kwa kuikata mikoko ni kukaribisha athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aliwaasa wananchi kuwa makini na watu wanaoharibu mazingira kwa sababu za athari zake ni kubwa kuliko faida.
Pia alimtaka sheha wa shehia hiyo kutoa taarifa mapema ili hatua ziweze kuchukuliwa na kuacha tabia ya kutosubiri kuharibiwa kwani waathirika wakuu ni wananchi.
Alisema lengo ni kuhakikisha mazingira yanatuzwa na Zanzibar inarejea katika uhalisia wake.
Ofisa Misitu, Ali Ussi Basha, aliwataka wananchi wa shehia hiyo kuhifadhi mazingira na kuendelea kupanda miti kwani ndio kimbilio kubwa la maisha ya mwanaadamu.
Jumla ya mikoko na mikomafi 1000 imepandwa katika shehia ya Fuoni Kibondeni ili kuhifadhi mazingira na kuyalinda maji ya bahari yasiingie katika maakaazi ya watu.