Na Kauthar Abdalla
CHANZO kikubwa cha migogoro kati ya waajiri na waajiriwa katika sekta binafsi ni ukorofi kwa baadhi ya wawekezaji wazalendo.
Imeonekana kuwa matatizo mengi yanayotokea katika sehemu za kazi ni maeneo ambayo wawekezaji wake ni wazalendo na sio wageni kwa sababu wengi wanafuata sheria na kanuni zilizowekwa.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Shangani, Kamishna wa kazi, Mashaka Kubingwa Simba, alisema wawekezaji wazalendo huwa wanajali zaidi maslahi yao badala ya maslahi ya wafanyakazi.
Alisema kamisheni imekuwa ikipokea migogoro mbali mbali inayohusu wafanyakazi na wamekuwa wakijitahidi kuitatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema ikishindikana inapelekwa mahakama kuu ambayo ina mamlaka zaidi ya kutoa uamuzi.
Aidha alisema tatizo ambalo linawakumba wafanyakazi kujiingiza katika migogoro hiyo ni uelewa mdogo zaidi wa sheria za kazi.
Aliwataka wafanyakazi wa sekta binafsi ambao wanalipwa mshahara kima ambacho hakistahili kutoa taarifa kamisheni ambayo kazi yake kubwa ni kusimamia sheria za kazi.