Na Amina Mmanga, Pemba
UONGOZI wa uwanja wa ndege Pemba, umeziomba mamlaka husika kuwapatia mashine maalumu za ukaguzi wa mizigo na abiria, ili kuepusha mizigo ya abiria kupekuliwa kwa mikono, kitendo ambacho huwakera abiria.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa uwanja huo, Rajab Ali Massoud, alisema tabia ya wafanyakazi wa uwanja huo kupekua mizigo kwa kuifungua, huwaudhi abiria wengi na wakati mwengine kutoa lugha zisizo nzuri.
Alisema kwa sasa wafanyakazi hao huwalazimu kuifungua mizigo ya abiria na kupekua na wakati mwengine husababisha migogoro na abiria.
Alisema wakati umefika kwa serikali kuharakisha ununuzi wa mashine hizo ili kuwa na uhakika wa kile kinachopitisha badala ya kuangalia mizigo kwa macho na mikono mitupu.
“Hivi sasa wafanyakazi wa uwanja huu wanalazimika kutumia mikono wakati wa kupekua mizigo ya abiria wanaosafiri kwa ndege, lakini tukipata mashine ndio suluhisho,” alisema.
Aidha alisema kuwepo uhaba wa wafanyakazi pamoja na baadhi ya vitendea kazi husababisha kutokufanya kazi zao kwa ufanisi.
Alisema kuanzia mwaka 2013-2014 idadi ya abiria wanaotumia uwanja huo imeongezeka kutokana na safari za ndege kuongezeka.
Mkuu wa ulinzi na usalama,Ali Sudi Ali, alisema ukosefu wa wafanyakazi pamoja na mashine ya kukagulia mizigo ya abiria ni kikwazo katika uwanja huo.
Alisema juhudi za kiomba serikali zimeshachukuliwa na hivi karibuni wanatarajiwa kupatiwa kifaa hicho lakini ni vyema serikali kuharakisha upatikanaji wa kifaa hicho.