Na Benedict Liwenga, Dodoma.
BUNGE Maalum la Katiba limepitisha marekebisho ya kanuni ili kuliwezesha kufikia hatua ya mwisho ya upigaji kura kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 2 mwaka huu.
Hatua hiyo ililenga kumaliza vikao vya Bunge hilo kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa sheria wa Oktoba 4 mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, wakati alipokuwa akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu uwasilishwaji wa azimio la kupitisha marekebisho ya kanuni za bunge hilo.
Alisema inakadiriwa kuwa wajumbe wasiopungua 480 wanatarajiwa kupiga kura na kutokana na kanuni zilivyokuwa kabla ya mapendekezo ya mabadiliko hayo ingechukua siku nyingi kukamilisha zoezi la upigaji kura kwa kupitia kifungu kwa kifungu.
“Kanuni zilivyo hivi sasa kama hatutafanya mabadiliko itachukua kwa wastani wa dakika kama mbili kwa kila mjumbe kupiga kura kwa kila kifungu ambapo kwa siku tutamia wastani wa dakika 960 kwa ibara moja, tunatarajia ibara zitakuwa 300,” alisema na kuongeza “kwa ibara hizo tungehitaji siku 300 kukamilisha zoezi hilo ambao muda huo utakuwa kinyume na utaratibu uliopangwa tutakuwa tunamaliza ibara moja kwa siku moja,” alisema.
Alisisitiza kuwa marekebisho yaliyofanyika yalilenga kuhakikisha kazi ya upigaji kura inakuwa rahisi na inamalizika katika muda uliopangwa wa kisheria wa siku 60.
Awali akiwasilisha maelezo ya marekebisho ya kanuni za bunge maalum kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya kanuni na haki za Bunge Maalum, Amon Mpanju, alisema kanuni zilizofanyiwa mabadiliko ni ya 36 na 38.
Alisema marekebisho hayo yatamwezesha mjumbe aliye nje ya maeneo ya Bunge kwa ruhusa ya maandishi ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba kupiga kura ya wazi na siri kwa njia ya nukushi na mtandao.
Alisema hatua nyingine ni kumwezesha mjumbe kupiga kura katika muda usiozidi siku saba kwa urahisi na ufanisi.
Akitoa ufafanuzi wa wajumbe walioko hijja, Sheikh Norman Jongo, alisema mjumbe anayetekeleza ibada hiyo hakatazwi kupiga kura ili mradi hajafikia hatua za mwisho wa ibada hiyo.
Wakati huo huo rasimu ya katiba mpya iliyopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba Septemba 24, mwaka huu.
Mabadiliko hayo yametangazwa na Katibuwa Bunge Maalum la Katiba, Yahya Khamis Hamad, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema uamuzi wa mabadiliko hayo umetokana na kufanyika kikao baina ya Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi.
Hata hivyo, alisema kazi ya uandishi wa rasimu hiyo imeshakamilika na kazi iliyobakia ni kuipitia kwa makini.
Aliongeza kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, inatarajia kukabidhiwa rasimu ya katiba mpya iliyopendekezwa Septemba 23, mwaka huu kutoka kwa Kamati ya Uandishi wa Bunge hilo.