Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

ZANAB, TLB zawakuna wafadhili

$
0
0
Na Salum Vuai
BAADA ya kuridhishwa na mafanikio yaliyopatikana katika Mradi wa Skuli inaoufadhili kupitia Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TLB), taasisi ya 'My Right' ya nchini Sweden imeamua kuongeza fedha katika awamu ya pili ya mradi huo.

Taasisi hiyo ambayo awali iliitwa 'SRF' kabla kubadilishwa na kupewa jina jipya la 'My Right', imeongeza fedha za mradi huo kufikia shilingi 200,000,022.

Fedha hizo hutolewa kwa ajili ya kuwawezesha watoto wasioona na maalbino ambao ama wameacha skuli au hawajapelekwa kabisa, kuandikishwa ili nao wapate haki ya elimu.

Akizungumza katika mkutano wa maofisa wa Jumuiya ya Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB) kutoka wilayani uliofanyika ofisini kwao Kikwajuni, mjumbe wa kamati inayosimamia mradi huo Zanzibar Fatma Djaa Chesa,  amesema katika awamu ya kwanza mradi huo ulipewa shilingi 190,000,000.

Alifahamisha kuwa, takriban watoto 100 wamenufaika na mradi huo kwa awamu ya kwanza ya miaka mitatu iliyoanza mwaka 2011 na kumalizika mwaka 2013, ambao wamepelekwa skuli pamoja na kupatiwa vifaa mbalimbali zikiwemo sare na viatu.

Akizungumzia utekelezaji wa awamu hiyo ya kwanza, Fatma alisema kwa upande wa Unguja, walikuwa wakifanyia kazi Wilaya ya Kusini, na kwa Pemba Wilaya ya Wete.
Alieleza kuwa, katika awamu ya pili, ZANAB imeamua kutanua wigo na kuingia Wilaya ya Kati na Kaskazini A Unguja, ambapo kwa Pemba Wilaya ya Wete itaendelea kuwa mlengwa mshiriki.


Hata hivyo, mjumbe huyo ambaye anakaimu nafasi ya mratibu Adil Mohammed aliyeko Dodoma kwenye Bunge Maalum la Katiba, alisema mradi huo unakabiliwa na changamoto kadhaa.

Aliitaja changamoto kubwa ni kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu wa ngozi (maalbino), awali walikuwa wakikataa kuwatoa watoto wao, kutokana na kushamiri kwa ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu kama huo huko Tanzania Bara.

Hata hivyo, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za kuwajengea mazingira mazuri watu wasioona na walemavu wengine, na kuitaka jamii izidishe ushirikiano ili kutetea haki za kundi hilo.

Mapema, akizungumza na washiriki wa mkutano huo, Naibu Katibu wa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) Jonas Lubago, alisema awali wadhamini wao SRF walikuwa wakitoa ruzuku kwa ajili ya kuendeshea shughuli za jumuiya zao Bara na Zanzibar, lakini kuanzia mwaka 2008 wameamua kutenga bajeti kwa ajili ya miradi maalum.
Lubago alieleza kuwa, kwa upande wa Tanzania Bara, awamu ya kwanza iliweza kuwafikia watoto 81, ambao sasa wanafurahia maendeleo mazuri katika skuli wengi wao wakiwa mabwenini.
Alieleza kuwa awamu ya pili ya mradi huo unaoendeshwa kwa pamoja na Chama cha Maalbino, ZANAB na TLB,  inaanza mwaka huu 2014 hadi 2017.  



Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>