Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Ali Mohammed Shein, amefanya uteuzi wa wajumbe wa bodi katika taasisi mbali mbali za serikali.
Uteuzi huo ulitangazwa mjini Zanzibar na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, ambapo alieleza kuwa ulianza rasmi Septemba 30 mwaka huu.
Walioteuliwa ni Dk. Issa Haji Ziddy, anaekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni Wakfu na Mali ya Amana, ambapo uteuzi huo umefanywa chini ya sheria namba 2 ya mwaka 2007 kifungu cha 5 (2) iliyounda taasisi hiyo.
Kwa upande wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Mwenyekiti anakuwa Kombo Hassan Juma, ambapo uteuzi wake umefanywa chini ya sheria namba 3 ya mwaka 2011 kifungu cha 4 (1)(a).
Dk.Mohammed Mwinyi Mzale, ameteuliwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ukuzaji Vitega Uchumi (ZIPA) chini ya sheria namba 11 ya mwaka 2004, kifungu cha 6(2) (a).
Kwa upande wa Shirika la Meli na Uwakala chini ya sheria namba 3 ya mwaka 2013 kifungu cha 10 (2)(a),Dk Shein, amemteua Kepteni, Abdulla Yussuf Jumbe, kuwa Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo.
Kwa upande wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), Dk. Shein amemteua, Ahmeid Sheikh Abdulrahman kuwa Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo.
Bodi ya Ushauri ya Mambo ya Nyaraka na Kumbukumbu, alieteuliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ni Amour Abdalla Khamis.
Aidha alimteua Mwalimu Haji Ameir, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na Salmin Senga Salmin kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bandari.