Na Khamis Amani
MAMLAKA ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) imewaomba wafanyabiashara wa kigeni kuvitumia vizuri vivutio vya Zanzibar kwa kuwekeza miradi yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA,Ndg. Salum Nassor, alisema Zanzibar ni visiwa vilivyojaaliwa kuwa na vivutio vingi na vizuri kwa uwekezaji, ambavyo vinaweza kukuza biashara.
Aliyasema hayo katika hoteli ya Double Tree Shangani mjini Unguja, wakati wa mkutano na wafanyabiashara wakubwa kutoka nchini Marekani wa VIP Safari.
Alisema vivutio vya Zanzibar vina mandhari nzuri kwa wawekezaji ambavyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara ikiwemo utalii.
Alisema ujio wa wafanyabiashara hao utasaidia kuitangaza Zanzibar kiuchumi na kiutalii pamoja na kukuza urafiki wa muda mrefu baina ya Tanzania na Marekani.
Hivyo aliwaomba wafanyabiashara hao kukubali kuwekeza miradi yao ambayo itasaidia kuondoa umasikini kwa kuwapatia ajira vijana, kuitangaza nchi pamoja na kuinua pato la taifa.
Balozi wa Tanzania mjini Washington DC, Balozi. Suleiman Saleh, alisema Tanzania ni nchi iliyojaaliwa na vivutio vingi vya utalii ikiwemo mbuga za wanyama na fukwe za bahari, ambazo vikitangazwa vinaweza kuwashawishi wawekezaji kuwekeza miradi yao.
Alisema, ubalozi wake umefanya jitihada kubwa za kuitangaza Tanzania ikiwemo Zanzibar kuvutia wawekezaji jambo ambalo linahitaji kuungwa mkono na serikali na wadau wote wa utalii.
Alisema katika kufanikisha hilo aliweza kuwafikisha wafanyabiashara wakubwa kukagua vivutio hivyo ambavyo vimeleta mafanikio katika suala zima la uwekezaji.
Alisema ujio wa wafanyabiashara hao unaweza kuleta tija katika sekta ya uwekezaji jambo ambalo linahitaji jitihada za Serikali katika kuimarisha ulinzi kwa wawekezaji, watalii na mali zao pamoja na kuweka miundombinu imara.
Nao wafanyabiashara hao walisema, wameridhishwa na vivutio vizuri vilivyopo Zanzibar na kuahidi kuwekeza miradi yao pamoja na kuitangaza nchi kiutalii.
Hiyo ni ziara ya tatu kwa wafanyabiashara wakubwa wa Marekani kufika nchini kwa ajili ya kukagua vivutio kwa ajili ya uwekezaji.