Na Mwanajuma Abdi, Dar es Salaam
SERIKALI ya Finland imekabidhi hundi ya shilingi milioni 150, kwa washindi 10 wa tunzo ya ubunifu wa mfumo wa habari na mawasiliano yanayorahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.
Hafla hiyo imefanyika jana katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia jijini Dar es Salaam, ambapo Balozi wa Finland nchini Tanzania, Sinikka Antila, alikabidhi hundi hizo mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Patrick Makungu, aliyemuakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa.
Alisema fedha walizokabidhiwa vijana 10 kutoka kampuni mbali mbali za ubunifu waliotengeza ‘software’ kupitia mawasiliano ya kompyuta na smart phone, ambazo zinarahisisha upatikanaji wa bidhaa mbali mbali kupitia TEHAMA.
Alisema serikali yake kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri wa Muungano Tanzania, wameanzisha mfuko wa kuwasaidia wabunifu ikiwa ni mradi wa kukuza maendeleo nchini hususani kwa vijana wajasiriamali.
Alisema malengo hayo yanakwenda sambamba na dira ya maendeleo ya Tanzania ya ukuaji wa kati wa uchumi ifikapo mwaka 2025, katika kuimarisha uzalishaji wa bidhaa katika sekta mbali mbali, hivyo kuwepo kwa wabunifu hao kutatoa fursa kwa wenzao kuajiri na kukabiliana na masoko katika ulimwengu wa utandawazi.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof.Patrick Makungu kwa niaba ya waziri wake, alisema ubunifu unasaidia kuzalisha ajira kwa vijana, ambapo fedha walizokabidhiwa zitasaidia kuzalisha ajira za heshima kwa wenzao.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Hassan Mshinda, alisema ubunifu huo utaisaidia jamii kununua bidhaa za biashara nje na ndani ya nchi kupitia sekta ya habari na mwasiliano (TEHAMA).
Nao washindi hao, walisema walijishindia fedha hizo baada ya kutengeneza software katika kompyuta na kuingiza taarifa za bidhaa kupitia teknolojia hiyo ambapo mtu aliyeko eneo lolote anaweza kujua habari ya bidhaa hiyo.