Na Kauthar Abdalla
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itahakikisha inazifanyia kazi changamoto zinazoikabili sekta ya usafiri wa anga ili kuimarisha usalama wa sekta hiyo.
Waziri wa Usafirishaji, Dk. Harison Mwakyembe, aliyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Mbwana Juma Mbwana, katika mkutano wa kwanza wa jumuiya ya vyuo vya usafiri wa anga uliofanyika hoteli ya Ocean View Kilimani Zanzibar.
Alisema pamoja na kuimarika kwa sekta hiyo katika miaka ya hivi karibuni bado kuna mambo kadhaa yanatakiwa kufanyiwa kazi ili kuchochea kazi ya maendeleo ya nchi.
Alisema usafiri wa anga ni moja ya sekta zinazopelekea ukuaji wa uchumi kwa haraka hivyo ukuaji wake na uimara wa miundombinu ya sekta hiyo ni lazima iendane na mahitaji ya kazi ya ukuaji wake.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa usafiri wa anga katika uchumi wa Afrika,Mawaziri wanaohusika na sekta hiyo waliazimia kuanzisha mikakati ya kitaifa,kikanda na bara zima ili kuhakikisha usalama wake kwa lengo la kuchangia sekta nyengine za uchumi hivyo umoja huo ni lazima uzingatie utekelezaji wa majukumu yake,” alisema.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Dk.James Diu, alisema mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na kutokuwa na wataalamu wa kutosha katika fani hiyo jambo ambalo linakwamisha harakati za kimaendeleo katika jumuiya na kushindwa kuendelea mbele.
Malengo mkakati ya mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania ni pamoja na kuwa na sauti ya pamoja ya vyuo wanachama na kuhimiza vyuo hivyo kuendeshwa kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.