Na Joseph Ngilisho, Arusha
WANANCHI zaidi ya 24,000 waishio vijijini wanatarajia kunufaika na mradi wa umeme wa j na upepo katika kipindi cha miezi 18 ijayo.
Hayo yalisemwa na Kamishana wa Nishati na Petroli, Hosea Mbise, wakati akikagua maonesho ya makampuni 57 mkutano wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) jijini Arusha.
Alisema kikubwa katika mkutano huo wanatarajia kuteuwa makampuni 20 kati ya hayo yalioshiriki maonesho hayo, baada ya kushinda, ili wapewe kazi ya kusambaza umeme vijijini ambako gridi ya taifa haipo.
“Umeme huo tunaamini utakuwa wa bei nafuu kwa wananchi wengi wa vijijini na utawaondoa katika lindi la umaskini,”alisema.
Aidha alisema makampuni hayo ambayo yatateuliwa kwenye mkutano huo, yataanza kazi mara baada ya kuteuliwa na ndani ya miezi 18 wananchi watajionea umeme umesambaa kwa kasi maeneo yao.
Alisema gharama za mradi huo ni shilingi bilioni 4.6, ambazo tayari zimetengwa kwa ajili ya kuwapatia makampuni 20 yatakayoshinda kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.
“Fedha hizi zitagawanywa kulingana na ukubwa wa kazi ya kampuni husika na kila kampuni itafanya kazi katika kijiji chake ili mradi wasambae maeneo tofauti nchi nzima,” alisema.
Naye mmoja wa washiriki wa maonesho hayo, Mkuu wa Idara ya Ufundi kwenye kampuni ya T&A Business Center Ltd, Mgogiley Fivawo, alisema endapo kampuni yake itashinda atasambaza umeme kwenye sekondari moja ya Rufiji na Vituo vya Afya viwili huko Rufiji.
Alisema eneo la Rufiji lina rasilimali nyingi za uchumi kama zao la biashara la korosho, samaki na minazi, lakini wananchi wengi hawana nishati ya umeme.