Na Asya Hassan
OFISA Tawala wilaya ya magharibi, Sabah Saleh, amesema kuanzishwa mabaraza ya watoto na wazee kutasaidia kuimarisha maendeleo yao.
Alisema hayo katika uzinduzi wa mabaraza hayo kwenye shehia ya Kiembesamaki katika hafla iliyofanyika viwanja vya sheha wa shehia hiyo.
Alisema kuwepo kwa mabaraza hayo ni chachu ya kuwawezesha kujua haki zao pamoja na kuwajengea uwezo watoto hao kuweza kuripoti matukio ya udhalilishaji yanayowakumba.
Alisema kumekuwa na matukio mengi mabaya yanayofanywa kwa watoto na yanashindwa kufikia mwisho na kupata haki zao za msingi.
Alisema kutokana na kukua sayansi na teknolojia kunasababisha vijana kukumbwa na matukio mengi hali inayosababisha kukosa haki zao.
Hata hivyo, Ofisa huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wazee washirikiane na vijana wao katika kufanikisha maendeleo ya mabaraza hayo na wasione kama watoto wao wanapewa mzigo.
Nae sheha wa shehia hiyo, Mwinyi Khatib Juma, alisema watoto wamekuwa wakishawishiwa mara kwa mara juu ya kujishirikisha katika makundi maovu hali inayopelekea kuacha maadili yao.