Na Kauthar Abdalla
IPO haja ya kurejeshwa malezi ya pamoja katika jamii pamoja na kuimarisha ndoa ili kutunza familia na watoto kuepukane vitendo vya udhalilishaji.
Mjumbe kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Zanzibar, Sharifa Maulid, alisema hayo katika kongamano la wazee juu ya hifadhi ya mtoto na mapambano ya udhalilishaji katika ukumbi wa hoteli ya Mazsons Shangani mjini Unguja wakati akiwasilisha mada ya udhalilishaji.
Alisema mfumo wa malezi kwa watoto umebadilika tofauti na ilivyokuwa zamani na kwamba ongezeko la talaka kwa wanandoa linachangia kwa kiasi kikubwa kudhalilishwa watoto kwani wanakosa matunzo yanayostahiki.
Aidha alisema vitendo vya udhalilishaji kwa watoto vinawaathiri kiakili, kimwili na kisaikolojia hali ambayo inampelekea mtoto kukosa haki zake za msingi.
Kaimu Mkurugenzi kijiji cha kulelea watoto yatima (SOS) Salum Abrahman Salum, alisema ni wakati sasa kwa taifa kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji.
Alisema kutokana na hali hiyo taifa halitakuwa na mtetezi na siku zote litakuwa tegemezi hali ambayo itapelekea kukosekana maendeleo endelevu nchini.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya taasisi na familia kuchukua madaraka waliyonayo kutatua kesi hizo kwa njia ya kienyeji.
Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo, walisema ni bora wakarudishwa walimu wenye hisia za kidini katika skuli za serikali na binafsi na katika vyuo vya madrasa ili wawafahamishe watoto juu ya mwenendo mzima wa maisha unavyokwenda.