Na Salama Salim, ZJMMC
ZAIDI ya wanyama 21,000 wamepatiwa chanjo ya kuwakinga na maradhi ya kichaa cha mbwa katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Maabara na Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Wanyama Zanzibar, katika Ofisi za Idara ya Huduma za Utabibu wa Mifugo, Dk. Warid Abdalla Musa, alisema kampeni ya kuchanja wanyama hao inatekelezwa kwa ufadhili wa Shirika la Kutetea Wanyama Duniani na Serikali Zanzibar.
Alisema maradhi ya kichaa cha mbwa yamekuwa yakiathiri mifugo kama vile mbuzi,ngo’mbe na paka na wakati mwengine kusambulia binaadamu.
Maeneo yaliyoathirika zaidi na maradhi hayo ni Ubago, Caheju na Koani kwa wilaya ya kati pamoja na Fuoni na Chuini kwa upande wa wilaya ya magharibi.
Aidha alisema maeneo mengine yalioathirika zaidi ni Donge na Zingwezingwe kwa upande wa mkoa wa kaskazini Unguja.
Alisema maradhi hayo yanasabishwa na virusi vinavyojuilikana kama NYSA vinavyoshambulia mishipa ya fahamu, tezi za mate na viungo vya uzazi ambapo dalili zake ni kubadilika tabia na mnyama kuwa mkali.
Alisema juhudi mbali mbali zinachukuliwa ili kudhibiti maradhi hayo ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa inayojuilikana kama ‘rabies vaccine’, ambayo hutolewa mara moja kwa mwaka pamoja na kutoa elimu juu ya udhibiti wa maradhi hayo.