Na Khamisuu Abdallah
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuibua masuala mbalimbali ya udhalilishaji wa kijinsia ili kuongeza uelewa kwa jamii.
Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari yaliyofanyika Ofisi ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (ZANAB), Msimamizi wa vipindi vya redio kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kanda ya Dar es Salam, Judica Losai, alisema ikiwa waandishi wa habari wataongeza uelewa na kuibua mambo mbalimbali ya udhalilishaji itawawezesha watunga sheria kutoa sheria madhubuti ambayo itatoa haki kwa wafanyaji wa vitendo hivyo.
Alisema ni vyema kwa wanahabari kujikita zaidi katika kuelimisha jamii masuala ya udhalilishaji ili jamii iweze kujitambua.
Aidha alisema lengo la mkutano huo ni kuimarisha zaidi masuala ya udhalilishaji na kutoa muamko kwa jamii kuhusu vitendo hivyo.
Kwa upande wake mwanachama wa chama hicho kanda ya Zanzibar, Sophia Ngalapi, alisema ni vyema kwa waandishi hao kuyafanyia kazi ipasavyo mafunzo watakayopewa na kuitumia vyema taaluma yao kwa kuandika habari za udhalilishaji ili vitendo hivyo viweze kuondoka.
Nao wanahabari wakichangia mada, walisema masuala ya udhalilishaji wa kijinsia yapo zaidi katika maskuli na vyuo vya madrasa huku sheria ikiwa ndio changamoto kubwa ya kuzorotesha uendeshaji wa kesi hizo.
Mafunzo hayo yameandaliwa na TAMWA na kuwashirikisha wanahabari kutoka vyombo mbali mbali.