Na Kija Elias, Siha
WAGONJWA wa kisukari wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, wanalazimika kutembea umbali wa kilometa 20,kutafuta matibabu kutokana na huduma hiyo kutolewa katika hospitali ya wilaya pekee.
Kufuatia hali hiyo, wameiomba serikali ya wilaya hiyo kuwasogezea huduma za afya katika maeneo yao.
Matibabu kwa wagonjwa wa kisukari inatolewa hospitali moja tu ya wilaya jambo ambalo limekuwa likisababisha wagonjwa kutembea umbali mrefu.
Katibu wa klabu ya wagonjwa wa kisukari wilayani hapa (DIABETIC), Halima Hamisi, alitoa ombi hilo katika hospitali ya wilaya ya Siha wakati akizungumza na umoja wa wanawake wa CCM.
Akizungumza na wagonjwa hao, Katibu wa UWT, wilayani hapa, Zeydani Mwamba, aliishukuru serikali kwa kuimarisha miundombinu katika hospitali hiyo ambayo imeanza kutoa huduma huku akiwataka wagonjwa hao kuwa na subira juu ya tatizo hilo.
Mratibu wa huduma za maabara wa wilaya hiyo, Zakaria Magoye, alikiri kuwepo tatizo hilo na kusema serikali itajitahidi kuweka kliniki za kisukari katika hospitali za wilaya.