Na Mwantanga Ame
Hatimae wajumbe wa bunge maalum la katiba, wamepitisha rasimu ya katiba inayopendekezwa, baada ya kupata theluthi mbili ya kura kutoka pande zote mbili za Muungano.
Furaha na nderemo zilihanikiza ukumbi wa bunge, baada ya Naibu Katibu wa bunge hilo, Dk. Thomas Kashilila, kutangaza matokeo ya kura zilizopigwa.
Shughuli za bunge zilisimama kwa muda kutokana na wajumbe kuanza kuimba nyimbo mbali mbali kwa furaha, baada ya Naibu Katibu huyo kumaliza kusoma kura za upande wa Zanzibar.
Akitangaza matokeo ya kura hiyo, Kashilila alisema theluthi mbili ya kura za Zanzibar imepatikana na baadae kuanza kusoma kura za upande wa Tanzania Bara.
Wasi wasi mkubwa ulikuwepo kwa kura za Zanzibar kama zingetimiza theluthi mbili baada ya baadhi ya wajumbe kupiga kura ya hapana na wengine kukataa baadhi ya vifungu.
Alisema wajumbe wa Zanzibar,walipaswa kuwa 219 na waliopiga kura walikuwa ni 154 huku wajumbe 65 wakikosa kupiga kura.
Alisema ili theluthi mbili ya Zanzibar iweze kupatikana kulihitajika kupatikana kura 146.
Akichambua matokeo hayo, Kashilila alisema katika sura ya kwanza yenye ibara ya 1 hadi 11, imepata theluthi mbili, sura ya pili yenye ibara ya 12 hadi 21 imepata theluthi mbili, sura ya tatu inayoanza na ibara 22 hadi 26 imepata theluthi mbili na hali kama hiyo ilijitokeza kwa sura nyengine zote.
Baada ya Naibu Katibu kusoma kura za ibara zote, ndipo Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, alipotangaza rasmi kupitishwa rasimu inayopendekezwa.
Akitoa maelezo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Endrew Chenge, alisema kutokana na matokeo hayo rasimu hiyo sasa itaitwa rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2014, ambayo itakwenda kwa wananchi kupigiwa kura.
Alisema bunge hilo limezipigia kura ibara zote kwa kuzingatia uwepo wa theluthi mbili katika pande zote za Muungano na ni dhahirisha kwamba rasimu hiyo imeungwa mkono.
Akitoa shukurani, Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, alisema kazi hiyo imemalizika ikiiacha Tanzania katika hali ya amani na utulivu licha yakujitokeza vitimbi vilivyokuwa vikiashiria kutaka kuvuruga amani.
Alisema wakati mchakato huo unamalizika, angetamani kuona serikali inawatengezea mazingira Watanzania wakati watakapopiga kura katika uchaguzi mkuu ujao, iende sambamba na upigaji kura wa katiba hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, alisema Tanzania imefanikiwa kujenga historia na itakuwa busara kwa Watanzania kuiunga mkono kwa sababu imejali maslahi ya makundi tofauti wakiwemo wanawake.
Aidha aliwataka Watanzania kupambanua pale yanapojitokeza matamko ya baadhi ya watu wanaojiita Wazanzibari wanaokataa Muungano kwa sababu sio wote wanaoukataa.
Aliwaomba wananchi wa kuepuka propaganda zinazoendelea kutolewa kwamba wajumbe wa bunge hilo wamepoteza fedha za wananchi.
Nae mjumbe mkongwe wa bunge hilo, mzee Kingunge Ngobale Mwiru, aliwataka wajumbe wa bunge hilo, kuacha kulumbana na wabunge waliotoka ama makundi mengine yanayoipinga katiba hiyo na badala yake waende kufanya kazi ya kuwashawishi wananchi kuipigia kura ya ndio.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alikanusha madai kwamba alikuwa akilipwa shilingi 7,000,000 ili kubadilisha kanuni za kuendesha bunge na kwamba hata angepewa angezikataa.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anna Makinda, aliwataka Watanzania kutambua kwamba umasikini hauwezi kuondoka kwa kuvutana kila wakati badala yake wajenge tabia ya kupendana.
Mjumbe wa bunge hilo, Hamad Rashid Mohammed, alisema haoni haja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kukubali kutumia katiba yenye viraka katika uchaguzi mkuu ujao na badala yake aharakishe kutumika kwa katiba mpya.
Nae John Cheyo, alieleza kufurahishwa na hatua iliyofikiwa na atakuwa tayari kuhakikisha katiba hiyo inaungwa mkono.
Nae mjumbe kutoka Chadema, John Shibuda, alisema yuko tayari kuitwa msaliti lakini kazi aliyoifanya kwa ajili ya kuwatetea wakulima, wafugaji na wavuvi imekamilika.
Nao viongozi wa dini wakitoa shukrani zao akiwamo Sheikh, Nouman Juma Jongo, walisema wanakubaliana na maamuzi ya Mwenyezi Mungu na kuumaliza mchakato huo kwa usalama.
Askofu mstaafu Dornad Mtetemele, alisema ni vyema Watanzania kuipokea katiba inayopendekezwa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wajumbe wa bunge hilo, Peter Serukamba, alisema kitendo walichokifanya kimewajengea historia kubwa kwa kuumaliza mchakato huo katika hali ya usalama na amani.
Upande wa kundi la 201, mjumbe Amon Mpanju, aliwapongeza wajumbe hao kwa kuandika katiba iliyozingatia haki za walemavu, wavuvi na wakulima mambo ambayo hayajawahi kuzingatiwa katika katiba iliyopita.
Nae Mjumbe Hawa Mchafu, akitoa shukrani kwa niaba ya wanawake na vijana,alisema ni vyemakwa vijana wa Tanzania kuiona katiba hiyo ni yao kwa sababu imezingatia Maslahi yao.