Na Bakar Mussa, Pemba
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Pemba, wametakiwa kufanya kazi kwa bidii na uwajibikaji.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi wa raslimali watu wa mamlaka hiyo, Rajab Talib Abdalla, wakati akizungumza na wafanyakazi wa mamlaka hiyo katika hafla ya kuwazawadia wafanyakazi bora.
Alisema katika kipindi kifupi kijacho mamlaka itaweka vifaa vya usalama katika uwanja huo.
Bado abiria wanaosafiri katika uwanja huo wamekuwa wakipekuliwa kwa kutumia mikono hali inayosababisha migogoro baadhi ya wakati.
Alisema miongoni mwa mikakati ya mamlaka katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kuwapatia mafunzo wafanyakazi wake wanaokaribia kustaafu, ili wanapomaliza muda wa utumishi wasiwe na hofu juu ya maisha yao.
Nae Meneja wa mamlaka ya uwanja wa ndege Pemba, Rajab Ali Mussa, alisema kumekuwa na ushirkiano mkubwa katika uwanja huo kati ya wafanyakazi na mawakala wa mashirika ya ndege jambo ambalo limeongeza kiwango cha abiria kutoka 250 hadi 300 kwa siku sawa asilimia 11.6.
Alisema ongezeko hilo limekwenda sambamba na kuwepo ndege 14 kwa siku na mashirika 18 ya ndege yanayotoa huduma.
Mzee Ali Juma, kutoka Jumuiya ya Cotwu Pemba, aliwasihi wafanyakazi wa mamlaka hiyo kuzidisha nidhamu katika kazi zao za kila siku.