Na Masanja Mabula, Pemba
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, Jaji Mshibe Ali Bakar, ameitaka jamii kuacha tabia ya kukimbilia mahakamani kupata haki kwa sababu kesi nyingi zinazofikishwa mahakamani zinaweza kutatuliwa nje ya mahakama.
Amesema Tume hiyo imeamua kutembelea maeneo yote ya Zanzibar kwa lengo la kutoa taaluma kwa jamii juu ya sheria ili kusaidia kupungua mrundikano wa kesi mahakamani ambazo baadhi yao hazina haja ya kufikishwa huko.
Akizungumza katika kikao kilichowashirikisha wafanyakazi kutoka taasisi za serikali na ninafisi mkoa wa kaskazini Pemba, alisema hakuna budi mwananchi anayetaka kupeleka shauri lake mahakamani kujitambua kabla hajaliwasilisha.
“Baadhi ya kesi zinazofikishwa mahakamani hazina mashiko, jambao ambalo linapelekea kesi kufutwa na baadae wananchi kulalamika,” alisema.
Aliitaka jamii kubadilisha kurejesha tabia inayopotea ya uaminifu hasa kwa wazee kutokana na kuongezeka vitendo viovu vinavyofanywa na kundi hilo.
Akizungumzia uhusiano kati ya wakili na mteja, Mwanasheria Khamis Mwita Haji, alisema lazima wakili aweze atunze siri za mteja wake na anapaswa kumweleza mwenendo mzima wa kesi yake.
Akichangia katika kikao hicho, Sheha wa shehia ya Mtemani Wete, Juma Mrisho Magogo, alisema bado baadhi ya wazazi wanawaonea aibu watoto wao na kwamba wanashindwa kuwambia ukweli kuhusu nyenendo zao.