Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

‘Muuguzi mmoja wa akili hutibu wagonjwa 100’

$
0
0
Na.Aboud  Hussein na Simai Mati
SERIKALI ya Zanzibar inakabiliwa na upungufu mkubwa wa waauguzi wa afya ya akili katika hospitali kuu ya wagonjwa wa akili ya Kidongochekundu, hali inayosababisha wagonjwa kupata huduma za chini mno.

Hilo limebainishwa jana na Ofisa wa Ustawi wa Jamii, ambaye pia ni Muunguzi katika kituo hicho, Saghira Mohammed Abdallah, wakati akizungumza na Zanzibar Leo, katika hospitali ya kuu ya wagonjwa wa akili ya Kidongchekundu mjini Unguja.

Alisema suala la wauguzi na tatizo la usafiri katika hospitali hiyo,ni moja ya changamoto kubwa inayoendelea kuwasumbua katika utoaji wa huduma.

Alisema kituo hicho kwa sasa kina wauguzi wanne, ambapo kwa uwiano kila muuguzi mmoja anahudumia karibu wagonjwa 100 kwa siku, badala ya muuguzi mmoja kuwahudumia wagojwa 20.
Kwa upande wa usafiri, alisema hospitali hiyo ina gari moja ambapo inapokosa mafuta kazi zinashindwa kufanyika.

Aidha alisema hospitali inakabiliwa na uhaba wa dawa hasa kwa wagonjwa wa nje hali inayosababisha matatizo kwa wagonjwa wa akili kuongezeka.

Alisema kila kidonge kimoja aina ya carbamazipine kina gharimu shilingi 200, ambapo mgonjwa mmoja anatakiwa kutumia mara tatu kwa siku, jambo ambalo humfanya mgonjwa kutumia takribani shilingi 1000 kwa siku.


Kwa ujumla alisema hospitali inakabiliwa na tatizo la kutoa matibabu bora kwa wagonjwa wa akili.

Nae Mratibu wa Afya ya Akili ya Jamii Kanda ya Unguja, Mohammed Joel, alisema tatizo la ugonjwa wa akili limekuwa kubwa Zanzibar na linasababishwa kwa kiasi kikubwa na matatizo ya kimazingira, kimwili na kijamii kama vile urithi, utumiaji wa dawa za kulevya na hali ngumu za maisha.

Alitoa wito kwa wanajamii na kwa wadau wengine kutokuwachukulia vibaya au kuwanyanyapaa wagonjwa wa afya ya akili, kwani kila mmoja anaweza kukutwa na ugonjwa huo katika mazingira tofauti, na sio lazima atumie dawa za kulevya.

Hospitali ya wagonjwa wa akili kwa sasa ipo kwenye maadhimisho ya siku ya wagonjwa wa akili duniani ambayo hudhimishwa Oktoba 10 kila mwaka.

Katika maadhimisho hayo kituo hicho kimeendesha shughuli mbalimbali tangu Oktoba mosi, zikiwemo usafi wa mazingira, darasa kwa wagonjwa wa nje, ziara za kiafya, kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na kilele chake kitaambatana na michezo ya aina mbalimbali kwa wagonjwa.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Kuishi na Skizofrenia’ (Living with Schizophrenia), inayomaanisha akili kuwa na mitazamo hasi na kutokujielewa katika hali ya kawaida, ambapo Shirika la Afya Ulimwenguni limeiweka kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanajamii kuishi na hali hiyo kwa usalama.


Kwa mujibu wa WHO, asilimia 26 ya watu wote ulimwenguni wanasumbuliwa na skizofrenia, asilimia 50 ya wagonjwa hawatibiki, kutokana na ugonjwa huo, na asilimia 90 ya wagonjwa wote ni kutoka katika nchi zinazoendelea.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>