Na Khamisuu Abdallah
MTOTO Shafik Shaisu Othman (10) mkaazi wa Fuoni, amefariki dunia wakati akiogelea katika bwawa la kuogelea liliopo katika bustani ya wanyama Zanzibar Park, wakati akisherekea sikukuu ya Eid el Hajj.
Akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Muembemadema, Kamanda wa polisi mkoa wa mjini magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, alisema tukio hilo lilitolea juzi saa 8:30 mchana na kusema kifo chake kilitokana na kuzidiwa na maji.
Alisema polisi wanaendelea na upelelezi ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Hivyo aliwataka wazazi kusimamia watoto wao wanapokwenda katika sherehe mbalimbali hasa za sikukuu na kuwashauri wamiliki wa bustani hiyo kuweka kima maalum cha maji kwa watoto na watu wazima ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.
Wakati huo huo Kamanda Mkadam alisema tukio jengine lilitokea Oktoba 7 mwaka huu saa 11:00 jioni wakati Adam Haji (22) mkaazi wa Magogoni alipofariki dunia wakati akiwa anafua.
Aidha alisema kifo cha marehemu huyo kilisababishwa na saruji ya nyumbani kwao kupata maji iliyosababisha kuteleza na kufariki dunia papo hapo.
Alisema uchunguzi wa awali unaonesha kifo cha marehemu kilisababishwa na umeme.
Alisema mwili wa marehemu ulipelekwa hospitali kuu ya Mmnazimmoja kwa uchunguzi na kukabidhiwa jamaa zake kwa mazishi.