Na Asha Salim, Pemba
WAVUVI katika wilaya ya Micheweni wametakiwa kuchukua tahadhari kubwa juu ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola hasa wanapokuwa dago nje ya kisiwa cha Pemba.
Tahadhari hiyo imetolewa na Maofisa wa Idara ya Uvuvi, wakati wakizungumza na wavuvi pamoja na wanajamii katika kijiji cha Shumba mjini, wilayani humo.
Walisema miongoni mwa watu wanaotakiwa kuchukua tahadhari juu ya maambukizi ya Ebola ni wavuvi wanaotoka na kuingia katika visiwa tofauti pamoja na kuacha tabia ya kuchukua wageni kiholela.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Sharif Mohamed Faki, alisema ugonjwa wa Ebola ni hatari na kwamba hauna chanjo wala tiba.
Alisema ni vyema jamii ikafuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya pamoja na kuacha tabia ya kusalimiana kwa kupeana mikono na watu wasiowajua wakiwa safarini.
Awali akitoa maelezo mafupi kuhusiana na njia za maambukizi ya ugonjwa huo, Ofisa Mipango Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Khalfan Amour Juma, alisema ni Ebola unaambukizwa kwa kugusa maji maji ya muathirika.
Aliwahimiza wavuvi kutokula wanyama pori hasa jamii ya kima na popo pamoja na matunda yaliyoliwa na kuachwa na wanyama hao.
Katibu wa kamati ya bandari ya Micheweni, Hussein Rashid Hussein, aliwataka wavuvi wenzake kuwa makini wakati wanapochukua wageni ili kujikinga na mripuko wa ugonjwa huo.