Na Mwanajuma Abdi, Dar es Salaam
RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Ali Hassan Mwinyi, amesema kuna kila sababu ya kumuezi hayati Mwalimu Nyerere, kwa kuwa alikuwa ni kiongozi wa mfano katika bara la Afrika kutokana na busara zake.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa alipofanya mahojiano na vyombo vya habari baada ya kumaliza mashindano ya Rotary Dar Marathon, katika viwanja vya Osterbay.
Alisema Mwalimu wa Nyerere alikuwa mstaari wa mbele kudumisha amani na kupinga ubaguzi wa aina yeyote.
Alisema ana kila sababu za kumpongeza kiongozi huyo, ambae alimsaidia katika kumnyanyua hadi akapata urais, jambo ambalo hakuwahi kulifikiria.
Alisema yeye alikuwa mwalimu kitaaluma lakini Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Mbunge na kumpa uwaziri mwaka 1970, jambo ambalo lilisaidia kubadilisha maisha yake.
Alisema kitendo cha kumteua kuwa waziri kilisaidia kumjenga kisiasa hadi kuwa Rais wa Tanzania.
“Mimi nilikuwa mwalimu kitaaluma sikuwa na ndoto za kuwa Rais wa nchi hii, bali nilikuwa na mawazo ya kugombania nafasi za kiongozi wa walimu lakini yeye ndie aliyenisaidia kunifikisha hapa,” alisema.
Aliwapongeza viongozi wa klabu za Rotary Dar Marathon kwa kuandaa mashindano hayo yenye lengo la kuleta maendeleo katika nchi, ambapo zaidi ya shilingi milioni 700 na vitu mbali mbali vilikusanywa.
Mapema Mkuu wa Rotary kanda ya Tanzania na Uganda, Harish Bhatt, alisema klabu sita za Rotary Dar es Salaam, zimeandaa mashindano hayo, ambapo fedha zilizokusanywa zitatumika kwa ajili ya kujenga kituo maalumu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.