Na Mwandishi wetu, Tabora
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Kikwete, amesema serikali imeanza kuchukua hatua kuandaa kura maoni kuhusu katiba mpya na kuwataka wananchi siku itakapofika wakafanye maamuzi.
Akizungumza katika sherehe za kumbukumbu ya kifo cha Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ambazo kitaifa zilifanyika Tabora, alisema hata hivyo, katiba inayopendekezwa ni bora kuliko katiba ya sasa.
Alisema katiba hiyo inatoa majubu sahihi kwa changamoto zilizopo sasa na kutoa mapendekeo ya kutatua changamoto za kesho.
Aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye kura ya maoni na kuiunga mkono katiba hiyo kwa kuipigia kura ya ndio.
Aidha aliwataka wananchi kuisoma katiba hiyo ibara moja baada ya nyengine na kuwatahadharisha kuepuka kuondolewa kwenye malengo yenye maslahi kwao na kubeba ajenda za watu wengine wenye maslahi yao binafsi.
Kuhusu rushwa, alisema serikali itaendelea na mapambano na kuwataka wafanyakazi kuwafichua viongozi wanaochukua rushwa badala ya kuwatukuza au kuwalinda na kufikiria kazi hiyo ni ya TAKUKURU pekee.
Kuhusu vita vya dawa za kulevya,alisema mapambano hayo ni magumu mno, ingawa kuna mafanikio yaliyopatikana.
Alisema zaidi ya watu 6,000 wamekamatwa wakisafirisha dawa za kulevya ingawa bado changamoto za kuwadhibiti ni kubwa kutokana na kubadilisha mbinu kila mara.
Aliwataka vijana kuacha kutumiwa kusafirisha dawa za kulevya au kutumia dawa hizo na kwamba serikali itaongeza mapambano kudhibiti uingizaji wa dawa hizo.
Alilipongeza Bunge Maalum la Katiba kwa uamuzi wake wa kusimamia kwa vitendo misngi iliyoachwa na Mwalimu Nyerere kuhakikisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuwa moja.
Kuhusu Ukimwi hasa mkoa wa Tabora, alisema asilimia tano ya wakazi wa mkoa huo wanaishi na ugonjwa huo ambapo watu watanao kila watu 100 wameambukizwa ugonjwa huo, kiwango ambacho alisema ni kikubwa.