Na Abdi Suleiman, Pemba
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Pemba, imeamua kuifanyia matengenezo barabara ya Chanjaani-Mkoani, kwa kuijenga kingo za kupitishia maji ya mvua, zitakazo gharimu shilingi 30,000,000.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisa Mdhamini wa wizara hiyo, Hamad Ahemed Baucha, alisema lengo la kujenga kingo hizo ni kuifanya barabara hiyo kuwa bora na imara.
Alisema kujengwa kwa mabega hayo ni mpango wa serikali kuamua kuzitengeneza barabara zake, kwa kuzipatia zabuni kampuni za kizalendo, ili wananchi walio katika barabara hizo kuweza kujiajiri.
Akizungumzia mikakati ya wizara yake, alisema ni kuhakikisha barabara zote zilizojengwa zinaimarika na kudumu kwa muda mrefu.
Alizitaja barabara hizo, kuwa ni Wete-Gando, Raha-Ukunjwi, Wete-Konde, Mchomanne-Kwale, ChanjaMjawiri-Tundauwa,Chanjaani-Pujini, Mtambile-Kngani, Mizingani-Wambaa, Kenye-Chambani, Bahanasa-Daya, Makungeni-Uwondwe, Mzambarau Takao-Pandani-Finya, Mzambarau Karim-Mapofu-Finya,Chwale-Kojani na Kipangani-Kangagani.
Akizunguzmia changamoto wanazokumbana nazo, alisema ni kuondolewa kwa alama za barabarani katika maeneo mbali mbali hali inayosababisha usumbufu kwa madereva wanaotumia barabara hizo.
Alisema changamoto nyengine, gari kumwaga mafuta barabarani na kusababisha barabara kuharibika.
Katibu wa Jumuiya ya wenye gari na madereva mkoa wa kusini Pemba (PESAT), Hafidh Salimu Mbarka, aliipongeza wizara hiyo kwa kujenga kingo hizo.
Alisema kufanya hivyo ni jambo zuri ambalo litaifanya barabara kuwa imara na kudumu kwa muda mrefu bila ya kuharibika.
Madereva wa gari za mkoa wa kusini Pemba, waliipongeza ya serikali kujenga kingo hizo kwa lengo la kuhifadhi barabara hizo.