Na Madina Issa
Watu watatu wamefariki dunia katika matukio tofauti katika mkoa wa mjini magharibi, akiwemo mtoto mchanga kutupwa katika ziwa la Mwantenga.
Kamanda wa Polisi mkoa wa mjini magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, aliwataja marehemu hao kuwa ni Khamis Ali Ame na Rajab Suleiman Salum (19).
Alisema marehemu Khamis Ali Ame alikufa Oktoba 9 mwaka huu saa 2:00 asubuhi Shaurimoyo ambapo kifo chake kilitokea baada ya kuanguka chini wakati akitembea kuelekea katika shughuli zake za kawaida.
Alisema marehemu alifikishwa hospital kuu ya Mnazimmoja kwa uchunguzi na baadae kukabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi.
Alisema tukio jengine limetokea Oktoba 8 mwaka huu saa 2:00 asubuhi katika bahari ya Kizingo ambapo iliokotwa maiti ya kijana aliyetambulika kwa jina la Rajab Suleiman Salum (19) mkaazi wa Taveta.
Alisema kifo cha marehemu kilisababishwa na kuzidiwa na maji alipokuwa akiogolea katika bahari hiyo.
Alisema mwili wa marehemu ulifikishwa hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa uchunguzi na kupewa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.
Tukio jengine lilitokea Oktoba 6 mwaka huu saa 12:30 usiku Nyerere ambapo mtoto mchanga wa kike wa siku moja, alikutwa ameshafariki dunia baada ya kutupwa katika ziwa la Mwantenga.
Alisema chanzo cha mtoto huyo kutupwa bado hakijajulikana na jeshi la polisi linaendelea na upelelezi.