Na Laylat Khalfan
Shilingi milioni 41 zimepatikana baada ya Kitengo cha Usarifu na Masoko, kusafirisha tani 11 za mwani kuanzia Julai 2013 hadi Juni 2014.
Mkurugenzi wa Idara ya mazao ya baharini, Mohammed Sudi Mohamed, alisema fedha hizo zinaingia kwenye mfuko wa hazina wa serikali.
Aidha alisema asilimia 80 ya uzalishaji wa mwani unafanywa kisiwani Pemba kwa sababu watu wengi wanajishughulisha zaidi na kilimo hicho wakiwemo wanaume.
Asilimia kubwa ya mwani uliouzwa nje ni mwembamba ambao ingawa hauna maslahi mazuri kwa wakulima lakini uzalishaji wake ni mkubwa duniani kote.
Ofisa wa mwani kutoka kitengo cha ukulima wa mwani Maruhubi, Hamisuu Maruzuk Yussuf, alisema kumekuwepo na athari mbalimbali za uharibifu wa misitu kunaokosababishwa na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kilimo hicho.
Pia alisema kuna tatizo la mmong’onyoko wa fukwe za baharini unaosababishwa na idadi kubwa ya watu wanaopita kila siku katika eneo moja kwa ajili ya shughuli za upandaji mwani.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wakulima wa zao hilo, alisema kuwepo kwa bei ndogo ya mwani kunawafunja moyo wakulima ikilinganishwa na kazi kubwa ya uoteshaji wa zao hilo.