Na Masanja Mabula,Pemba
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika skuli ya sekondari ya Limbani, amefariki dunia papo hapo na wengine watano kulazwa hospitali ya Wete, baada ya kugongwa na gari katika eneo la Chasasa.
Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa saba za mchana baada ya gari aina ya Scudo yenye namba za usajili Z109 BA ambayo ilikuwa ikiendeshwa na dereva Abrahman Khamis Juma (45 ) ikitokea Chake Chake kuwagonga na kusababisha kifo cha mwanafunzi huyo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Katibu wa hospitali ya Wete, Juma Mahamoud Badru, amekiri kupokea maiti ya mwanafunzi huyo pamoja na majeruhi wengine watano ambao wanaume ni wanne na msichana mmoja.
Alimtaja mwanafunzi aliyefariki kuwa ni Haitham Abdalla Hassan (18) ambapo wenzake waliojeruhiwa ni Fatma Othman Hamad (18) ambae pia ni mwanafunzi wa skuli hiyo, Massoud Said Juma (42), Ali Ahmed (55), Suleiman Juma Hamad (52) na Bakar Juma Bakar (26) ambao wameumia sehemu za kichwani.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,Kamanda wa polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Shakhan Mohamed Shekhan, alisema tayari majeruhi Suleiman Juma Hamad, amesafirishwa kwenda Muhimbili wakati Fatma Othman Hamad amesafirishwa kwenda
hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani.
Akielezea ajali hiyo, alisema baada ya gari hilo kumgonga mwanafunzi huyo liliacha njia na kueleka upande wa pili wa barabara na kuwagonga watu wengine.