Na Mwanajuma Abdi, Dar es Salaam
Takwimu za Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa,(UNICEF), zinaonesha takribani watoto wa kike 8,000 wanakatisha masomo kila mwaka nchini kutokana na kupewa ujauzito.
Mkurugenzi Mtendaji wa KIWOHEDE, ambae pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupinga Ndoa za Utotoni (TCEMN), Justa Mwaituka, alisema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika siku ya mtoto wa kike duniani, inayoadhimishwa kila Oktoba 11.
Alisema mujibu wa UNICEF watoto hao wanakatisha masomo sambamba idadi ya watoto wa kike wanaofaulu elimu ya msingi kwenda sekondari kukatisha masomo na kuolewa wakiwa na umri mdogo.
Alisema sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoafiki mtoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 15, haifai na imepitwa na wakati na kuiomba serikali kuifanya mabadiliko ili kuwalinda watoto wa kike.
Aidha alisema kuna ongezeko kubwa la watoto wa kike wanaosafirishwa kutoka vijijini na kuletwa mjini kwa ajili ya kuendelezwa kielimu lakini matokeo yake mabinti hao wamejikuta katika wakati mgumu kwa kufanyishwa kazi za ndani bila ya malipo stahiki na wengine kudhalilishwa.
Alisema hali hiyo inasababisha mabinti wengine kutoroka kutoka kwa waajiri wao na kuanza kuishi mitaani na hivyo kurubuniwa na kujiingiza katika biashara za ngono na baadhi yao kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.
Alitoa wito kwa vyombo vya habari kuwa makini wanaporipoti matukio ya ukatili wa watoto kwa sababu wakati mwengine utoaji wa taarifa unawavunjia haki zao.