Na Haji Nassor, Pemba
Mkuu wa wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Suleiman Salim, amesema sio kweli kwamba kisiwa cha Pemba hakijapiga hatua ya kimaendeleo, kama baadhi ya wanasiasa wanadavyodai wanapokuwa majukwaani.
Alisema kabla ya kuwasili Pemba, alikua na hakika kwamba ndani ya kisiwa hicho hakuna maendeleo yoyote yaliofikiwa na alikuwa anaamini serikali haijafanya lolote.
Alisema hayo wakati akizungumza na Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba,Mwanajuma Majid Abdalla, Mkuu wa wilaya ya Chake Chake, Hanuna Ibrahim Massoud na baadhi ya watendaji wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Idara Maalum za SMZ mjini Chake Chake.
Alisema sasa anaamini kwamba maneno ya wanasiasa yamekuwa ya upotoshaji mkubwa, na kuona kwa macho yake kwamba kisiwa cha Pemba kinan’gara kimaendeleo ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara.
Alisema hakuna hata wilaya moja ya Pemba ambayo haikukamilika kwa asilimia 90 muindombinu ya barabara, maji safi na salama, huduma za afya na elimu, na kuzipita baadhi ya halmashauri za mkoa wa Tanga.
“Maendeleo nilioyaona Pemba yako juu kuliko hata wilaya yangu ya Kilindi,” alisema.
Mapema Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla, alisema kwa sasa katika mkoa wake hakuna eneo ambalo ni kiwazo kwa upande wa miundombinu ya barabara, afya na elimu.
Mkuu wa wilaya ya Chake Chake, Hanuna Ibrahim Massoud, alisema wapo wanasiasa wanaopenda kusema uongo badala ya kuzungumzia uhalisia.
Akitoa taarifa fupi kwa ujumbe huo wa watendaji 10 kutoka mkoani Tanga, Ofisa Mdhamini Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Pemba, Saleh Mbaruok Omar, alisema halimashauri na mabaraza ya miji yamekua yakifanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Ujumbe huo ulitembelea miradi mbali mbali iliojengwa na mabaraza ya miji na halimashauri ikiwa ni pamoja na soko la Mkanyageni, soko la Qatari mjini Chake Chake, halimashauri za Mkoani, Chake Chake, Wete na Micheweni.